Wednesday, May 10, 2017

VITU MUHIMU VYA KUJUA KATIKA MASUALA YA MISINGI

Haleluya mtu wa Mungu, karibu katika mwendelezo wa masomo yetu. Kuna masuala au vitu vya kufahamu unapotaka kufanya maombi ya toba katika misingi ambavyo angalau vitaweka msukumo ndani yako wa kukusukuma kufanya maombi ya toba katika misingi, na leo tukaone kwa sehemu na tutaendelea tena siku nyingine. Bwana Yesu asifiwe

03. 01. Uhalali wa misingi

Misingi inaweza kuwa halali au ya uonevu; Biblia inasema tulikuwepo kabla ya kuumbwa kwa misingi ya dunia hii hivyo Mungu alipotaka kuleta ufalme wake hapa duniani, au alipoamua kutanua na kupanua ufalme wake wa mbinguni ili kuudhihirisha kwa namna ya kimwili alitengeneza mazingira kwanza (yaani eneo la kufikia msingi) ambayo ufalme wake utafikia na utaanzia kama mwanzo wa maisha au kama msingi wa ufalme wake na maisha ya watu wake. Mwanzo wa kuanzia ambako kulikuwa na utukufu wake, Uungu, uweza, umiliki na utawala wake au uzima katika yote ili uwe mwendelezo wa maisha ya baadae tokea katika msingi huo. Lakini dhambi iliingia katika msingi huo (Edeni) na kuanza kuachilia na kuzaa vitu tofauti (mauti) na vilivyokusudiwa tangu mwanzo (uzima) Warumi 5:12, Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi;

Misingi inapata uhalali kwa kujengwa, au kusimikwa au kuwekwa rasmi na wahusika tofauti kama; wakuu wa ukoo au familia, wakuu wa dini, eneo au nchi, viongozi juu ya eneo wanayotawala, ndugu. Wahusika hawa wanaweza kusimika au kuweka uhalali wa misingi kwa njia mbalimbali kama vile; sadaka, agano, kiapo, laana na kujenga mfumo wa maisha unaogusa vizazi au uzao wa baadae na hali yao ya maisha. Sadaka itanena juu ya wote walio ndani ya familia hiyo, ukoo, kanisa, eneo au himaya husika. Agano linagusa, linafungamanisha au ndani yake linabeba au linatawala maisha ya uzao wa aliyelifanya au aliyeanzisha msingi huo wa kiagano. Laana inafuatilia tokea kizazi husika mpaka vijavyo na kuachilia vitu vilivyobebwa ndani yake ili kuwapata walio ndani msingi huo kilaana. Na kiapo kinamfunga yeye aliyeapa na wote walio chini yake, katika utawala au umiliki wake au himaya yake.
Mfano wa 01
Ibrahimu aliingia katika agano na Mungu aliye hai, yeye kama baba wa familia yake na ulimwengu mzima. Sadaka aliyotoa iligusa maisha ya familia yake na ulimwengu mzima. Pia agano alilolifunga na Mungu aliye hai liligusa maisha ya familia yake kwa ujumla na ulimwengu wote mpaka kuuleta ulimwengu wote, lugha, kabila na mataifa katika agano jipya, yaani kwa Yesu Kristo. Maana yake Ibrahimu alikuwa na nafasi ya kutengeneza mazingira ya aidha kubarikiwa au kutokubarikiwa juu ya familia yake nzima na ulimwengu wote. Msingi ni mwanzo au chimbuko la baraka au laana.
Mfano wa 02
Ukisoma kitabu cha Ezekieli 21:19-23, Tena, mwanadamu, ujiwekee njia mbili, upanga wa mfalme wa Babeli upate kuja; hizo mbili zitatoka katika nchi moja; ukaandike mahali, upaandike penye kichwa cha njia iendayo mjini. Utaagiza njia, upanga upate kufikilia Raba wa wana wa Amoni, na kufikilia Yuda katika Yerusalemu, wenye maboma. Maana mfalme wa Babeli alisimama penye njia panda, penye kichwa cha njia hizo mbili, ili atumie uganga; aliitikisa mishale huko na huko, akaziuliza terafi, akayatazama maini. Katika mkono wake wa kuume alikuwa na kura ya Yerusalemu, kuviweka vyombo vya kubomolea, kufumbua kinywa katika machinjo, kuiinua sauti kwa kupiga kelele sana, kuweka vyombo vya kubomolea juu ya malango, kufanya maboma, na kujenga ngome. Jambo hili litakuwa kwao kama uganga wa ubatili, mbele ya macho yao waliowaapia viapo lakini ataufanya uovu ukumbukwe, ili kwamba wakamatwe.

Biblia inatuonesha wazi kabisa juu ya mkuu wa eneo, mtawala, kiongozi au mfalme wa Babeli akifanya matambiko na kuapa juu ya eneo lake na watu wote walio ndani ya umiliki na utawala wake ili liwe kama uovu kwao ukumbukwe daima na wakamatwe maana yake watawaliwe, watumikishe, walaaniwe au wawe chini yake ili awatawale kama atakavyo.

Viongozi au watawala wa kidunia yaani kisiasa wengi wanafanya maagano, viapo na matambiko ya namna ya mfalme wa Babeli ili wapate ushindi, nafasi, ushawishi, kupendwa na kibali mbele ya watu wanaowatawala na kuwatiisha chini ya nguvu zao na ndo maana wanauza ardhi za wananchi, mikataba mibovu, uongozi mbovu ulio katika misingi ya giza, mipango na sera mbovu zenye kuwaumiza na kuwatesa watu walio chini yao. Mungu anayo mipango mizuri ya watu wake ya kuwapa tumaini, njia sahihi za kuwapeleka watu wake katika amani, maelewano, umoja na mafanikio ndani ya Kristo Yesu. Hivyo omba toba juu ya msingi wa uongozi wa eneo lolote ulilopo hata kama unaishi hapo kwa mda mfupi ili utengeneze msingi wa uongozi, umiliki na utawala katika Mungu aliyehai ndani ya Yesu.

Mfano wa 03
Kuna baba mmoja ambaye aliamua kufanya biashara ya mbao katika msitu wa Mpanda- Rukwa. Ili uingie katika msitu huo, ufanye kazi zako vizuri na ufanikiwe kulikuwa na kanuni na taratibu za mila na desturi za mahali pale ambapo ilibidi uwaone wazee wa eneo lile ili wakueleze yakupasayo. Baba huyo aliingia katika kutekeleza taratibu na kanuni zao kwa kutoa sadaka na kiapo ambacho kilimhusisha yeye binafsi, familia yake na mifumo ya maisha yao yote. Baada ya muda mke wake alianza kuugua magonjwa ya ajabu ambayo kila akienda  kupima hospitali hawaoni tatizo, alikuwa anahisi mwili unawaka moto, miguu kama vile anakanyaga juu ya misumari inamchoma mpaka anashindwa kutoka ndani, anaumwa mgongo kila siku. Watoto wote walianza kuugua magonjwa ya ajabu mara kuishiwa maji mwilini, upofu, pia kielimu wote walikuwa wanashindwa licha ya kupelekwa katika shule kubwa zenye mazingira mazuri ya watoto kushinda lakini walikuwa wakirudia rudia. Mtoto wa mwisho alikuwa kama taahira hivi, ambako alifika darasa la sita akiwa hajui kusoma na kuandika vizuri lakini ana uwezo wa kutaja wachezaji wa timu za mpira za hapa Tanzania na wachezaji wa ulaya bila kukosea.
Maana yake baba aliingia agano na viapo vilivyomgusa yeye binafsi, familia nzima na mifumo ya maisha yao yote. Ili wawe huru ni lazima kuachilia, kunyunyizia na kumwaga damu ya Yesu katika msingi ili kufuta uhalali wake uliopatikana kwa njia ya sadaka, viapo na maagano. Damu ya Yesu inalipa gharama ya sadaka hiyo, inavunja maagano na viapo ili familia na maisha yao yawe huru ndani ya Kriso Yesu kwa njia ya damu yake Yesu Kristo.
Huwezi kuondoa uhalali wa misingi pasipo kibali, agizo au uhalali wa kuiondolea. Misingi iwe halali kwamba ilisimikwa na watu au iwe ya uonevu tu wa adui shetani, zote zinafutiwa uhalali wake na kuondolewa kabisa kwa njia ya damu ya Yesu aliye hai ili kutengeneza msingi mpya ulio bora ndani ya Kristo Yesu.

03. 02. Sababu za kuwepo kwa misingi (motives or reasons behind)

Sababu zinazopelekea kuanzishwa au kuwekwa kwa misingi fulani zinatofautiana. Inawezekana misingi inalenga mtu binafsi, jinsia, familia nzima, ukoo mzima, eneo la kiongozi kulingana na ngazi husika, wanafunzi fulani au wote ndani ya mipaka ya shule au chuo, kondoo au waumini walio chini ya mtumishi fulani, mfumo mmojawapo (au mifumo yote ya maisha) ambao ukiguswa na mifumo mingine itaguswa moja kwa moja au kwa namana  moja ama nyingine.
Inawezekana msingi uliosimikwa ulikusudiwa ufanye kazi kwa kipindi fulani, majira au wakati fulani. Mfano; kwa ngazi ya familia au ukoo, mtu akifikia hatua/umri wa kuoa au kuolewa, mtu anapochanua kiuchumi aidha afe, awehuke au afilisike, mtu akiingia katika ngazi fulani ya kielimu, kufariki kwa nafasi fulani ya uzao ndani ya familia au ukoo labda kila mtoto wa kwanza au mtu fulani akifa vitu fulani ndio vianze kulipuka au kufanya kazi au ndio vianze kuonekana kama vile magonjwa ya urithi, mtu anapookoka au kuanza kumtumikia Mungu ndio upinzani na vita vinapoanza na kuinuka juu yake kukataliwa na ndugu, walezi , kanisa na waumini.
Msingi unaanzishwa au unajengwa ili uwe mwendelezo (urithi) mpaka ghafla kuingilie nguvu ya kuvunja huo mnyororo (chain), kubomoa, kuharibu na kung¢oa msingi huo ili vilivyokuwa vimekamatiliwa au vimefungiwa ndani yake viwe huru kwa Neno la Mungu aliyehai. Yeremia 1:9-10, Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.

03.03.  Malengo ya msingi

Kusudi la kujenga msingi mbele yako ni nini? wanaweka nini wanapoujenga msingi leo kwa ajili ya maisha yako ya baadae? Sababu za kusimamisha msingi mbele yako zipo kadhaa kama:
Kukuzungushia wigo ili ukitaka kuvuka ukutane na ukuta (mipaka ili usivuke) yaani vizuizi, vikwazo katika eneo fulani ili uzungukie humo humo kimaisha na kihuduma. Lengo la kukuwekea ukuta mbele, wigo au uzio ni usione mbele, uone giza tu, ukate tamaa, urudi nyuma, ujione huwezi, hufai, huna maana. Ukuta; ni kuziba mahali unapotakiwa upaone ili usipaone au unapotakiwa kwenda au kuvuka ili usivuke. Lengo ni uishi au ukae ndani ya eneo hilo hilo au mfumo huo huo ili uendelee kuona yale yale kama kuonewa, kudharauliwa ugumu n.k.
Kukutafakarisha au kukufikirisha yaliyo ndani ya msingi uliomo, ufahamu, akili, fikra, na kuamini hujengwa katika vitu unavyoona, unavyosikia na unavyoishi. Mfano; ukiishi katika familia au ukoo uliozungukwa na vifo, magonjwa, kutooa, au kuolewa, ulevi, kuabudu miungu, na kutopiga hatua kimaisha aidha kielimu au kiuchumi, lazima huwezi kuona sababu ya kukusukuma kuvuka au kutoona sababu ya kutokutofautisha na mfumo wa maisha uliokuzunguka na wengine wanaokuzunguka. Mpaka neema ya Mungu aliye hai ikuzukie au uone nuru ya kukusaidia kuona mbali, kuona tofauti na hali ilivyo.
Kukujengea mfumo uliopofushwa ndani yako ili uone na useme kulingana na upofu ulio nao au uliotiwa ndani yake. Maamuzi juu hali ya maisha ya baadae yanasukumwa na unavyoona, unavyosikia, unavyofikiri au unavyotafakari kwa kuangalia hali au changamoto zilizopo bila kujua zimeletwa na nini au chanzo chake ni nini au chimbuko, kiini ili ushughurike na chanzo au msingi wa tatizo. 2Korintho 4:3, Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.


Kwa hiyo kazi ya damu ya Yesu inaponyunyiziwa katika misingi inabadilisha na kubatilisha malengo ya misingi ya giza kama wigo na kuta zinayeyushwa mbele yake, utatafakarishwa na nguvu mpya, roho mpya au uhai uliomo ndani ya damu ya Yesu, kujengewa msimamo thabiti ndani ya Kristo. Damu ina Roho ya uhai ndani yake ambayo inapoingia au kuachiliwa mahali ghafla unaanza kuona ramani mpya ya maisha, picha mpya, uelekeo mpya na neno la Bwana la kukuvusha ambalo halitarudi bure. Jifunze kuachilia, kunyunyizia na kumwaga damu ya Yesu aliyehai juu ya msingi wa maisha yako, familia, ukoo na eneo ulilopo ili kubatilisha kila hila na makusudio yaliyo kinyume na haja ya moyo wako ndani ya Yesu na mapenzi ya Mungu aliye hai juu ya maisha yako ya baade. 


NB. Haleluya mtu wa Mungu aliyehai, sasa unaweza ukafanya maombi ya toba kwa kufuta uhalali wa misingi kwa kutumia damu ya Yesu, kuvunja malengo ya misingi ya giza juu yako na familia au ukoo wako na kufuta sababu zozote zilizopelekea kuwepo kwa misingi ya giza katika maisha yako binafsi, familia, kanisa, au eneo unaloishi.

Pia tutaendelea na vitu vingine kwa neema ya Mungu, Mungu aliyehai katika Kristo Yesu atupe neema ya kujifunza na kuomba ili yawe yetu katika jina la Yesu Kristo. Amen

2 comments: