Wednesday, May 24, 2017

UWEZA NA NGUVU ILIYOMO NDANI YA DAMU YA YESU JUU YA MISINGI NA INAVYOGUSA HALI YA MAISHA YA WATU YA BAADAE

Na Mosses Benedict
Mawasiliano +255 762 371 383


Haleluya mtu wa Mungu aliyehai, tumekuwa tukijifunza somo linalohusu masuala ya misingi angalau kwa kuingia ndani kidogo kidogo kadiri ya neema ya Mungu, karibu sasa tuendelee na nguvu iliyoko ndani ya damu ya Yesu, vitu inavyofanya katika misingi ikiwa wewe mwombaji umeomba maombi ya toba katika misingi
kuwa nami..............

Tunapozungumzia damu, hatuizungumzii tu damu kama kimiminika tunavyojua, ila kwa jicho la ndani au la kiroho tunazungumzia uhai uliomo ndani ya damu, siyo tu damu ila uhai uliomo ndani ya damu. Uhai ni roho inayoishi, inayotenda kazi. Tunapozungumzia damu ya Yesu tunazungumzia uhai au roho ya Mungu iliyomo ndani ya damu yake, hivyo tunapoachilia, nyunyizia au tunapomwaga damu ya Yesu katika eneo lolote, mfano juu ya ardhi, madhabahu, malango au vifungo, katika ulimwengu wa roho tunakuwa tunaachilia uhai au Roho itendayo kazi iliyomo ndani ya damu ya Yesu aliyehai ili itende kazi ambayo tunakuwa tukitamka wakati wa kuomba.
Mahali popote palipo na damu ujue kuna roho fulani inayotenda kazi, kwa hiyo tunapofanya maombi ya toba katika misingi kwa jina la Yesu Kristo na katika damu ya Yesu maana yake tunaachilia Uungu wa Mungu, nguvu zake na uweza uliobebwa ndani ya damu yake ili ikatende kazi katika misingi husika ili tuwe huru katika maisha yetu ya baadae kwa njia ya damu ya Yesu aliye hai.
Zifuatazo ni baadhi ya sababu zinazoweza kumsukuma mtu kufanya maombi ya toba kwa kutumia damu ya Yesu katika misingi. ( au kwanini tunafanya maombi ya toba katika Misingi)
01. Ondoleo la dhambi na uovu uliopelekea uhalali wa misingi ya ufalme tofauti kusimamishwa
Efeso 1:7, Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.

Dhambi ni mlango wa ufalme wa adui, giza kumiliki na kutawala mahali alipoingia. Kumbuka misingi kama misingi inasimikwa na kupata uhalali rasmi kwa ruhusa kabisa na watu tofauti tofauti kama; mtu binafsi, ndugu yeyote, mzazi, kiongozi, watumishi kwa ngazi mbalimbali toka ngazi ya familia mpaka ngazi ya kitaifa.

Kwa hiyo damu ya Yesu inafuta dhambi, kosa, uovu, hatia na mashitaka yaliyofanyika huko mwanzo na kuruhusu dhambi ianze kutenda kazi. Inawezekana dhambi au uovu umechukua muda mrefu na kugharimu au kutaabisha maisha ya watu kwa muda mrefu, lakini damu isiyo na hila wala mawaa inapoachiliwa, inafuta kabisa na kuondoa uhalali wake na kuruhusu sasa ufalme wa Mungu aliyehai kuanza kutenda kazi ndani ya Kristo Yesu. Hivyo ukinyunyizia damu ya Yesu katika misingi jambo mojawapo linalokuwa linafanyika katika ulimwengu wa roho ni kufuta na kuondoa uhalali wa nguvu za giza juu ya maisha yako.
02. Kunena mema katika misingi
Ebr 12:24, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili. 1Petro 1:2, kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani na ziongezwe kwenu

Dhambi inapofutwa na kuondolewa mahali ilipoingia inatengezeza mazingira ya kumpa nafasi Mungu aliyehai au tunamkaribisha Yesu aliyehai katika msingi huo ili kuanzisha mfumo mpya, utawala mpya na umiliki mpya wa uzima na Nuru ambao unaanza kuachilia uzima katika maisha ya mtu binafsi, familia, ukoo au eneo

Maombi ya toba juu ya misingi kwa kunyunyiza damu ya Yesu yanaachilia vitu vipya vilivyo ndani ya Kristo Yesu na kuachilia uhai katika maisha ya mwombaji na eneo analoombea.
03. Kututenganisha na mfumo na ufalme tuliomo
Wana wa Israeli waliishi chini ya utumwa, taabu, shida, dhiki, mateso na kutumikishwa kwa muda mrefu pia hali ya kimaisha ilikuwa mbaya chini ya utawala na umiliki wa ufalme wa Farao uliokuwa juu yao na hali ya maisha yao.

Mungu aliposikia vilio vyao alijibu na kuwapa maelekezo ya kuwasaidia kwa kumtumia mtumishi wake Musa kuwa  wachinje mwana kondoo na kupaka damu yake katika miimo ya milango ya nyumba zao, ili iwe alama ya kuwatambulisha kuwa kila nyumba iliyopakwa damu katika miimo ya milango na mizingiti ni nyumba ya wana wa Israeli, ili mharibu au malaika wa Mungu asije akaingia ndani akawaua na kuwaangamiza. Lakini nyumba ambayo haijapakwa damu ya Yesu katika miimo na mizingiti ya milango ya nyumba yaani nyumba za wana wa Misri, malaika wa kuharibu aingie katika nyumba zisizo na damu katika milango ili kuua na kuangamiza waliomo ndani. Kwa hiyo damu ya mwanakondoo ilitumika kama ishara katika ulimwengu wa roho kutambulisha nyumba zilizopakwa damu katika milango ya wana wa Israeli ili kuwatambulisha ili waokolewe na wawe huru yaani wasiuawe wala kuangamizwa.Unapoachilia au kunyunyizia damu ya Yesu katika misingi inakutambulisha na inakutenganisha na mfumo wa maisha uliokuwa ukiishi, umiliki, utawala na hali ya maisha yako uliyokuwamo, na kuanzisha utawala mpya, umiliki na hali mpya juu ya maisha yako ya baade ndani ya Kristo Yesu.
04. Kuachilia uweza na nguvu iliyomo ndani ya damu ya Yesu ili kutenda kazi yake.
Ayubu 18:16-17, Chini, mizizi yake itakaushwa; Na juu, tawi lake litasinyaa. Kumbukumbu lake litakoma katika nchi, Wala hatakuwa na jina mashambani. Ukombozi yaani uzima katika maisha ya mtu, nguvu na uweza iliyomo ndani ya damu ya Yesu inapoachiliwa katika msingi wowote inafutilia mizizi yote, mapando yote, shikilio la ngome zilizoko ndani ya msingi huo Mizizi na shina vikiondolewa, vikichimbwa, kuvunjwa na kungolewa inapelekea na matawi yaliyokuwa yakionekana kuanza kunyauka, na kutoweka kwa hiyo matokeo ya kuwepo kwa nguvu za adui kama hali fulani ngumu iliyokuwa katika misingi hiyo inaanza kuachia katika maisha ya mtu binafsi, familia, ukoo, eneo, taasisi au katika utumishi na uhuru unaanza kutokea katika maisha anayoishi na anakoelekea. Isaya 37:25, Nimechimba na kunywa maji, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri.

Damu ya Yesu inaachilia roho ya Mungu itendayo kazi ambayo inafuatilia mizizi ya nguvu za giza ili kuichimbua, kuiondoa, kuikausha na kuingoa ili pawe huru kwa ajili ya ufalme mpya au nguvu hiyo mpya iliyo ndani ya damu ya Yesu. Maombi ya toba katika misingi kwa kunyunyizia damu yenye ya Roho ya Mungu aliyehai iliyomo ndani ya damu ya mwanae Yesu Kristo, ile Roho inafuatilia maagano, laana, viapo na sadaka ili kufuta uhalali wa msingi huo, pia nguvu iliyo ndani ya damu ya Yesu inaharibu, inabomoa, inaangamiza na kungoa kila mzizi na pando la ufalme wa adui na kuachilia nguvu mpya iliyo ndani ya Kristo Yesu juu ya hali ya maisha ya baadae tokea katika msingi uliojengwa ndani ya KristoYesu. 
05. Upatanisho  
Rum 3:22-25, ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa.
 Damu ya Yesu inatusafisha, inatuosha na inafuta dhambi, makosa, uovu, hatia, mashitaka, matokeo ya dhambi na gharama za dhambi zilizo juu yetu. Tunarehemiwa na kuzidi kutakaswa kwa Roho ya kweli iliyo ndani ya damu na kutuletea tena upatanisho katika madhabahu yake na ufalme wake wa Mungu aliye hai. Kol 1:13-14, 20-22, Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi. na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni. Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa;katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama;

Damu ya Yesu inapotutakasa inatutoa katika misingi ya adui, inatuhamisha na kutubadilisha kwa kuhuishwa na roho mpya iliyoko ndani ya damu ya Yesu na kutuweka katika ufalme wake na katika kiti chake cha enzi
Efe 2: 1-2, 5-6, 21-22, Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.

Tunapofanya maombi ya toba katika misingi iliyoharibika au iliyo chini ya utawala wa adui, nguvu na uweza iliyoko ndani ya damu ya Yesu yaani roho atendaye kazi ndani ya Kristo inatuchukua, inatunyakua, anatutoa katika ufalme wa adui na kutuhamisha ili kutuingiza katika ufalme wa Mungu baba mwenyezi kwa kutupatanisha kwa njia ya msalaba katika Kristo Yesu.
Weka maoni, mapendekezo au ushauri wako, katika kusaidia kukuza na kuboresha madhabahu hii ya Bwana.

Ubarikiwe sana

No comments:

Post a Comment