Saturday, May 6, 2017

Umuhimu au Malengo ya meza ya Bwana


By. Mwl MOSSES BENEDICTO 0762371383
Ni nini umuhimu wa meza ya Bwana? ni kwanini tushiriki meza ya Bwana? nini faida ya meza ya Bwana? Kuwa na nami katika somo hili/.............

     
       01.   Kumwingiza kila mshiriki katika agano.
Ukisoma baadhi ya maandiko katika biblia utaona hili jambo au jukumu ambalo linafanywa na makuhani waliopewa dhamana au mamlaka ya kuwaingiza washiriki katika agano kwa njia ya meza ya Bwana haijalishi washiriki wanajua kuwa kuishiriki meza ya Bwana kunawaingiza katika agano au hawajui, wanapenda kwa mioyo yao au hawapendi.

Kutoka 24:3,6-8, Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote. Mathayo 26:26-28, Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 1Kolintho 11: 23-25, Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.

Ukisoma kitabu cha kutoka, maandiko yanatuambia mtumishi wa Mungu aliyehai Musa alisimama kama kuhani kuwafundisha wana wa Israeli juu ya sheria ya Mungu wa Israeli, aliwaelekeza namna ya kuishi, aliwapa maagizo yote aliyoyatoa mbele za Mungu wao, Musa aliwafundisha mpaka wakaelewa kwa akili zao, fikra zao na mioyo yao na wakajipambanua, wakajihoji, wakajitafakari na walipoelewa juu ya mafundisho na maelekezo juu ya kanuni na taratibu zilizo ndani ya agano analotaka kuwaingiza ndipo wakaitikia wakasema tutii na kutenda sawasawa na maagizo au sheria ya Bwana Mungu wao. Kwaiyo Musa alihakikisha anawaelekeza namna ya kuishi maisha ya ndani ya agano wanaloliingia.

Yesu alitwaa mkate akaumega  akasema twaeni mle huu ndio mwili wangu, na akakitwataa kikombe akashukru akawapa akisema nyweni nyote katika hiki maana hii ndio damu ya agano imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Unaona Yesu mwenyewe kama kuhani mkuu akiwafundisha na kuwaelekeza wanafunzi wake na inaonekana aliwafundisha mpaka wakaelewa, maana mahali pengi katika biblia Yesu alikuwa akiongea jambo au akiwafundisha  na wasipoelewa wanafunzi wengi au baadhi yao walikuwa wakimuuliza, wengine walikuwa wakisemezana wao kwa wao na wengine wakinungunika, ile kwamba walikaa kimya na kufuata maelekezo waliyokuwa wakipewa lazima walielewa somo. Kama wasingeelewa pengine wangemuuliza maswali kadhaa kama, ivi kweli inawezekanaje Bwana mkubwa hii divai iwe damu ya agano? Hii divai inawezezaje kufuta au kuondoa dhambi? Tangu lini divai ikamwagika kwa ajili ya wengi au ni mithari mpya? Una maana gani kutwambia hii ni damu ya agano wakati sisi tunaiona kabisa kwa macho yetu ni divai na pengine wanajua aliyeitengeneza au ilikonunuliwa, Lazima wangeuliza. Maana yake Yesu kama kuhani mkuu aliwafundisha mpaka wakaelewa kuwa kikombe wanachokinywea au divai wanayoinywa kama ishara ya damu ya Kristo inawaangiza katika agano jipya ambalo hawajawahi kuishi, ni agano linalowaondolea dhambi na kuwaingiza katika maisha mapya yasiyo ya dhambi maana yake dhambi haitaonekana tena miongoni mwao waishirikio meza ya Bwana.

Agano wanaloingia ni la agano la kuachilia uzima ndani yao katika Kristo Yesu, amani, furaha, upendo halisi na umoja kwa kila anayeishiriki meza ya Bwana, wanaanza kuishi sheria mpya ndani yao, matendo mapaya na maisha ya Ufalme wa mbinguni ambao na Nuru ndani yao wamejifungamanisha nao, wamejiambatanisha, wamejitiisha na  wamejiweka chini ya umiliki na utawala wa Mungu aliyehai katika Kristo Yesu.
Kumbuka hili jambo ni la kiroho, na katika ulimwengu wa roho kuna falme mbili yaani Ufalme wa Mungu aliyehai katika Kristo Yesu na pia ufalme wa shetani, na kila ufalme ulio katika ulimwengu wa roho ungependa uwavute watu kuelekea kwake, uweke watu chini ya umiliki na utawala wake, na njia mojawapo ya kuingiza nafsi na roho za watu chini ya umiliki halali ni kwa njia ya agano na hasa agano la kidamu, kwaiyo Mungu aliyehai katika Kristo anatumia meza ya Bwana kuwaingiza watu katika agano, na shetani naye anatumia meza ya bwana kuwaingiza watu katika agano ili amiliki na atawale nafsi na roho zao. Kwaiyo kumbuka kuombea meza ya Bwana popote pale kwa kuachilia damu ya Yesu ili watu wanaoishiriki meza ya Bwana waingie katika agano na Mungu aliyehai katika Kristo Yesu. Haleluya!! haleluya watu wa Mungu aliyehai. 

02.  Kuhuisha au kuua utu wa ndani wa mshiriki.

1Kolintho 10:3-5, wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. 1Kolintho 11:29-30, Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala.. Ufunuo 3:1b, Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa. 2Kolintho 4:3-4, Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu. Kolisai 2:13-15, Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.

Mtumishi wa Mungu aliyehai Paulo anawambia Wakolintho kuwa miongoni mwao kuna baadhi ambao waliishiriki meza ya Bwana na sasa wameangamia, wamelala, wadhaifu na hawawezi tena katika yale waliyokuwa wakiweza kabla ya kuishiriki meza ya Bwana. Na katika kuangamia kuna makundi kadhaa ya walioangamia, waliolala, waliodhaifu na walio hawawezi;

v     Kuna walioangamia kwasababu waliula mkate na kukinywea kikombe bila ya uhalali wa kukinywea au bila ya uhalali wa moyo wa kuishiriki meza ya Bwana na kwasababu hiyo hasira ya Bwana ikawaka juu yao na kuwaangamiza.
v     Kuna waliokuwa na uhalali wa kuishiriki meza ya Bwana lakini baada ya kuishiriki hawakuifuata sheria, maagizo na taratibu za Bwana wao ikapelekea hasira ya Mungu mwenye wivu kuwaka juu yao.
v       Kuna walioishiriki meza ya mashetani hivo roho chafu, roho za pepo wabaya na waharibifu na nguvu za giza  zikawaua na kuwaharibu utu wao wa ndani.
Ushirika mtakatifu ni tukio linalowahusu watakatifu ambao lazima mioyo yao iwe imembeba Kristo ndani yao ambaye wanaenda kuula mwili wake na kuinywa damu yake. Hata kama ndani umekufa kitabu cha Wakolisa kinatuambia tulikuwa tumekufa kwa sababu ya makosa yetu, hatia, mashitaka, madeni, maovu yaliyotupata kwasababu ya anasa tulizozitenda. Lakini Yesu alipokufa msalabani alitusamehe na akafuta hatia zilizokuwa juu yetu na akatufufua utu wetu wa ndani na kutuhuisha ili tuwe hai katika Yeye, kwa namna ambavyo na vipawa na karama vilivyokuwa vimekufa ndani ya mtu vilifufuliwa ili vitende kazi iliyohai. Kwaiyo unaposhiriki meza ya Bwana kwa kukinywea kikombe cha damu ya Yesu inakuhuisha utu wa ndani yako kwasababu kumbuka jambo hili, ndani ya damu ya Yesu kuna Roho yake itendayo kazi, au kuna Roho ya uzima, Roho mtakatifu, Roho wa Mungu aliyehai kwaiyo unapoinywa damu ya Kristo unaingiza Roho yake ndani yako ambayo inaenda kuosha, kusafisha, kutakasa viungo vya ndani kukuhuisha na kukufufua utu wako wa ndani.
Sheatani naye anatumia meza ya mashetani kuachilia roho zake zinazoingia ndani ya mshiriki wa meza iyo kuua utu wake wa ndani, kutia unajisi macho na kuyatia upofu macho ili mtu asione tena vitu vya rohoni ambavyo alikuwa akiviona kabla ya kunajisika ndani kwa kuingiza damu iliyobeba nguvu za giza ndani yake, kuziba masikio na kuyanajisi ili mtu asisikie sauti ya Mungu wake ambayo sauti hiyo huwa na maelekezo ndani yake ya kumsaidia yule anayesikizishwa sauti ya Mungu aliyehai, kufanya moyo kuwa mzito na mkaidi au mgumu na wa kijiwe kwasababu nguvu za giza zinaharibu moyo na kupandikiza mapando na mbegu mbaya, kupofusha fikra za mtu ili asitafakari yaliyo mema juu ya Bwana Mungu wake bali atafakari ubaya, uovu na uasi.
Hali hii inapelekea kuua utu wa ndani wa washirika au kanisa linakuwa na watu ambao ndani yao wamekufa, wamelala, wamepoa, wamepoteza mwelekeo na vipawa na karama zimepoa ndani yao kwa sababu ya kushiriki kikombe na kunywa divai ambayo imebeba nguvu za ngiza ndani yake, na ndio maana unaweza ukakuta kanisa la Wakolintho kwa nje ni wapendwa wazuri tu katika mavazi, misuko ya nywele kwa mabinti na wanawake na nama ya kunyoa kwa vijana. Lakini mwenendo wao, tabia zao, lugha zao na kuishi kwao hakuna tofauti na wapagani, maana matendo ni yaleyale. Kwaiyo shetani ametumia meza za mashetani kuua utu wa ndani walio ndani ya kanisa la leo kama alivyoua na kuangamiza wapendwa wa kanisa la Kolintho.  Haleluya haleluya!!!
    Ø  Unasema naongea kitu gani, kaangalie matendo, tabia na mwenendo wa wapendwa wa kanisa la leo, angalia miongoni kiwango cha kumtumikia Mungu wanayekusanyika ni wa ngapi kama wengi wao sio tegemezi, hawawezi hata kujiombea kama vile Yesu hakuwafia. Jiulize mwenyewe alafu ujijibu moyoni mwako.

03.  Kuachili uhai ulio ndani ya damu ya Yesu kwa ajili ya ukombozi.

Zekaria 9:11, Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji. Waefeso 1:7, Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Wakolisai 1:13-14, Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; Yohana 4:10,13-14, Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai. Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.

Maandiko yanatuambia katika kitabu cha Zekaria kuwa kwasababu ya damu ya agano Mungu atawatoa watu wake waliofungwa na waliofichwa katika mashimo yasiyo na maji maana yake yenye ukame, mateso, magonjwa, mahangaiko na kilio na akawapeleka katika eneo lenye uheri, uzima, amani, utulivu, mapumziko na shibe na kuwapa maji ya uzima wa milele ambayo kila anywae hataona kiu tena ya matendo ya dunia hii. Mungu anasema ” nimewatoa” maana yake amewahamisha katika eneo walilokuwepo na kuwapeleka eneo lingine, amewabadirishia mahali walipokuwa. Pia maandiko yanatuambia katika kitabu cha Wakolisai kuwa alituokoa katika nguvu za giza maana yake katika mashimo yasiyo na maji, makaburi na magereza na kutuhamisha toka katika ufalme wa giza na kutuingiza katika Ufalme wake ndani ya Kristo Yesu ambao ndani ya Yesu kuna ukombozi kwasababu ya masamaha ya dhambi tunayoyapata kwa kuoshwa na damu ya Yesu.

Biblia inatumbia kuwa Mungu anawakomboa watu wake katika mashimo na nguvu za giza zilizo wafunga, wataabisha, watumikisha na kuwatesa kwa kuwasamehe dhambi zao ili kuondoa uhalali wowote ulio juu yao na kuwafungua vifungo vyao, kuwaponya magonjwa yao na kuwaweka huru katika Ufalme wa mwana wa pendo lake. Pia anapowapeleka katika Ufalme wa mwana wake anawapa maji ya uzima ambayo yanawahuisha ndani yao, yanaachilia hofu ya Mungu aliyehai, nguvu mpya ndani yao, mapenzi mapya na nafasi mpya ya Bwana Mungu wao. Maji hayo yanakata kiu ya dhambi iliyokuwa ndani yao, hamu na misukumo ya dunia hii inakauka ndani yao na anasa zinakauka ndani yao na kufanya kuanza maisha mapya ya uhai mpya unaopatikana kwa njia ya kuinywa damu ya Yesu na maji Yake yaliyo hai.

Kwaiyo lengo mojawapo la Mungu aliyehai kuanzisha meza ya Bwana na kuwapa jukumu hili watumishi wake hasa makuhani ni kukomboa watu wake toka katika mashimo na nguvu za giza kwa damu ya Yesu Kristo. Haleluya haleluya watu wa Mungu aliyehai !!!!!!

*      Sasa unaweza ukajiuliza peke yako na kutafakari, kama kuna meza ya mashetani unafikiri inawafanyaje watu kama sio kuwafunga vifungo, kuachilia roho za magonjwa, kuwataabisha watu na kuwatumikisha katika maisha yao?
*      Je, unaonaje ukiamua kuombea suala la meza ya Bwana ili kila watu wanapoishiriki ipate kuwaponya na kuwahuisha ndani yao katika jina la Yesu Kristo, kama unakubali kuombea suala hili- Mungu aliyehai akutie nguvu katika Kristo Yesu na akubariki.


04.  Kuachilia Roho ya usharika au umojakwa washirikio meza ya Bwana.

Kolisai 1:20-22, na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni. Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; Mathayo 26: 27-28, Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Kutoka 24: 3, Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Yohana 11:52, 15:9, 17:22-24, Wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja. Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu.

Katika maandiko hapo juu natamani tuchomoe baadhi ya maneno ya kutusaidia kulingana na lengo letu la meza ya Bwana kuachilia Roho ya usharika au umoja kwa watu wote ambao Yesu alikuja kwa ajili yao ambao sio tu kwa taifa moja bali awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika ili wakae pamoja na wawe wamoja, wakae katika upendo utakao achilia umoja miongoni mwao na wote kuwapatanisha na nafsi yake  kama vile Yesu na Baba yake walivyo na umoja na wakamilike katika umoja ili ulimwengu wote upate kujua kuwa Mungu anawapenda watu wake.

Soma kwa kurudia rudia maneno haya mpaka uone hali ya umoja unaotakiwa kuwepo ili kuwaleta watu pamoja katika Kristo Yesu na kazia hasa kwa maneno yaliyokolezwa , “na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake. Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu kwa matendo yenu mabaya amewapatanisha sasa katika mwili wa nyama yake kwa kufa kwake ili awalete ninyi mbele zake watakatifu wasio na mawaa wala lawama. Akakitwaa kikombe, akashukuru akawapa akisema Nyweni nyote katika hiki kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana na hukumu zake zote watu wote wakajibu kwa sauti moja wakasema Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda., Wala si kwa ajili ya taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja. Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi kaeni katika pendo langu. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao nawe ndani yangu ili wawe wamekamilika katika umoja; Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu.”

Ukisoma maandiko ya Neno la Mungu aliyehai katika Kristo Yesu utamuona Yesu mwenyewe anasema kuwa ni damu anayoimwaga kwa ajili ya wengi ili kuwakusanya watoto wa Baba yake waliotawanyika na kuwaleta pamoja ili wawe na umoja katika utukufu wake, pia Yesu akae ndani yao ili wakamilike katika upendo na umoja kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, familia, kusanyiko au kanisa zima ndani ya Kristo kwa Mungu wao.
Maandiko yantuambia amekusanya watu na kuwapatanisha katika mwili wa Kristo ili awalete wote mbele ya watakatifu wasio na hila wala mawaa ndani yao, maana yake kanisa lenye watu wenye utakatifu ndani yao ambao utakatifu uko ndani yao kwasababu ya kumbeba Yesu aliyemtakatifu ndani yao ambaye kwa sababu ya utakatifu huo anaachilia utakatifu kwa wote ivo kusanyiko zima kuwa na Roho moja ndani yao ambayo itawafanya watafakari sawa, waone sawa. Na utakatifu Aliouweka ndani yao ndio unaowaleta pamoja mbele za Mungu aliyehai pamoja na watakatifu wengine. Haleluya haleluya mtu wa Mungu aliyehai!!!

Mtumishi wa Mungu aliyehai katika Kristo Yesu- Paulo anatuambia inapotoea ndani ya familia, kanisa au eneo kukawa na hali ya matengano, majivuno, hila, mafarakano, kutoaminiana, kudharauliana na kuona wewe ndo umeoka na wengine hawajaokoka, masengenyo na kusemana vibaya ujue miongoni mwenu kuna jambo ambalo limewatenganisha, limewavuruga na kuwatapanya na sio Injili ya Kweli bali ni matokeo ya mapokeoa na mashauri ya kibinadamu au ya ulimwengu huu na sio Mungu aliyehai katika Kristo Yesu.

1Wakolinthi 1:10-15,  Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo? Nashukuru, kwa sababu sikumbatiza mtu kwenu, ila Krispo na Gayo; mtu asije akasema kwamba mlibatizwa kwa jina langu.

Kwaiyo lengo la Yesu kuanzisha meza ya Bwana kwa wanafunzi wake ili awapatanishe wao kwa wao, na wao kwa Mungu ndani Yake ili wawe na upendo halisi, umoja na usharika na alipoondoka aliwapa jukumu la kuunganisha watu wa mataifa yote, maeneo yote, hali zote, kabila na lugha zote katika utukufu wa Mungu aliyehai. Lakini shetani naye anatumia suala la meza ya mashetani kuachilia na kupandikiza roho za mafarakano ndani ya mioyo ya watu, hila, utengano, mipasuko, majivuno n.k

Kwasababu hiyo hebu tujiulize maswali haya pamoja juu kusudi la Yesu la kuwambia kunyweni nyote ili mwe na umoja;
v  Kulingana na mtazamo wako binafsi unafikri ni kwanini kuna dini zaidi ya moja, na hata dini moja ndani yake pia unakuta kuna madhehebu mengi na kila dhehebu lina taratibu tofauti na lingine licha ya kila dhehebu linasema tunamwabudu Mungu mmoja?
v  Kama yesu aliwapa kikombe wainywe damu yake walio wengi ili wawe na usharika mmoja na nia moja ndani yao sawa sawa na nia iliyokuwa ndani Yake, kwanini ndani ya kanisa moja unaweza ukakuta kuna mipasuko, kusemana vibaya, kuchukiana mfano miongoni mwa watumishi, viongozi wa kanisa, kwaya na vikundi vingine vilivyomo ndani ya kanisa husika au kwanini mioyo yao haiku pamoja ?
v  Unaelewa nini au alimaanisha nini mtumishi wa Mungu aliyehai Paulo alipokataza utengano,hila,  majivuno na kujisifu kuwa mimi ni wa Paulo, huyu ni wa Apolo na yule ni wa Kefa ilihali wote ni wa Kristo. Ina maana gani katika maisha tunayo yaishi kwa hapa duniani katika kizazi cha leo.
NB; Kuwepo kwa dini tofauti tofauti na madhehebu na vikundi mbalimbali ni jambo jema kabisa ili kuutangaza Ufalme wa Mungu aliyehai katika Kristo Yesu, lakini wanafanya nini ndani yake hiyo hali au yanayoendelea ndio ambayo Paulo anawashangaa watu wa Kolintho. Haleluya haleluya mtu wa Mungu aliyehai!!! 


Mungu wetu aliyehai katika Kristo Yesu na akubariki kwa baraka za rohoni na mwilini kwa kufuatilia somo hili linalolenga kuongeza kiwango cha umakini unapoamua kuishiriki meza ya Bwana. Mtu wa Mungu naomba utambue kuwa maarifa haya ni kwa sehemu hivo changanya na kile ulichokuwa nacho, soma maandiko juu haya masuala, soma vitabu vya watumishi mbalimbali waliopewa neema katika hili eneo, sikiliza mahubiri mbalimbali na ingia katika maombi ili Roho mtakatifu akupe maarifa zaidi ya kukusaidia ndani ya Kristo Yesu. Pia endelea kufuatilia masomo mengine tunayojaliwa na Mungu kwa neema yake anayotupa ili kuaachilia kwa njia hii ya mtandao. Tuomeane, na  NEEMA YA MUNGU IWE JUU YAKO.



11 comments:

  1. Mwenyezi mungu akubariki na akuagizie roho mtakatifu ili akufundishe zaidi Nawe uje utufunze na sisi, kwa maana..(warumi 8:28) AMINA

    ReplyDelete
    Replies
    1. Amen. Mungu akupe neema ya kuomba ili kwa pamoja tukue katika neema yake.

      Delete
  2. AMEN.Mungu aliyehai atuinue sote ktk jina la Yesu Kristo aliyehai.

    ReplyDelete
  3. Mke na mume wakitengana wanaruhusiwa kushiriki meza ya Bwana?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hawarusiwi kumeka mkate.mbaka wapatane kwanza.

      Delete
  4. Mafundisho mazuri kabisa,ubarikiwe

    ReplyDelete
  5. Playtech | Casino Software Provider - DRMCD
    Playtech provides the most 포천 출장마사지 detailed 부산광역 출장안마 casino software for 보령 출장안마 the gaming industry, providing top-quality games to clients all 대구광역 출장안마 over the world. Our 익산 출장샵 range of casino solutions

    ReplyDelete
  6. Meza ya Bwana na itufanye imara Tena. Amen

    ReplyDelete
  7. Ubarikiwe sana mtu wa Mungu

    ReplyDelete