Wednesday, May 17, 2017

Mwendelezo wa mambo ya kufahamu yanayohusiana na misingi

03.03.  Malengo ya msingi

Kusudi la kujenga msingi mbele yako ni nini? wanaweka nini wanapoujenga msingi leo kwa ajili ya maisha yako ya baadae? Sababu za kusimamisha msingi mbele yako zipo kadhaa kama:
Kukuzungushia wigo ili ukitaka kuvuka ukutane na ukuta (mipaka ili usivuke) yaani vizuizi, vikwazo katika eneo fulani ili uzungukie humo humo kimaisha na kihuduma. Lengo la kukuwekea ukuta mbele, wigo au uzio ni usione mbele, uone giza tu, ukate tamaa, urudi nyuma, ujione huwezi, hufai, huna maana. Ukuta; ni kuziba mahali unapotakiwa upaone ili usipaone au unapotakiwa kwenda au kuvuka ili usivuke. Lengo ni uishi au ukae ndani ya eneo hilo hilo au mfumo huo huo ili uendelee kuona yale yale kama kuonewa, kudharauliwa ugumu n.k.
Kukutafakarisha au kukufikirisha yaliyo ndani ya msingi uliomo, ufahamu, akili, fikra, na kuamini hujengwa katika vitu unavyoona, unavyosikia na unavyoishi. Mfano; ukiishi katika familia au ukoo uliozungukwa na vifo, magonjwa, kutooa, au kuolewa, ulevi, kuabudu miungu, na kutopiga hatua kimaisha aidha kielimu au kiuchumi, lazima huwezi kuona sababu ya kukusukuma kuvuka au kutoona sababu ya kutokutofautisha na mfumo wa maisha uliokuzunguka na wengine wanaokuzunguka. Mpaka neema ya Mungu aliye hai ikuzukie au uone nuru ya kukusaidia kuona mbali, kuona tofauti na hali ilivyo.
Kukujengea mfumo uliopofushwa ndani yako ili uone na useme kulingana na upofu ulio nao au uliotiwa ndani yake. Maamuzi juu hali ya maisha ya baadae yanasukumwa na unavyoona, unavyosikia, unavyofikiri au unavyotafakari kwa kuangalia hali au changamoto zilizopo bila kujua zimeletwa na nini au chanzo chake ni nini au chimbuko, kiini ili ushughurike na chanzo au msingi wa tatizo. 2Korintho 4:3, Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.

Kwa hiyo kazi ya damu ya Yesu inaponyunyiziwa katika misingi inabadilisha na kubatilisha malengo ya misingi ya giza kama wigo na kuta zinayeyushwa mbele yake, utatafakarishwa na nguvu mpya, roho mpya au uhai uliomo ndani ya damu ya Yesu, kujengewa msimamo thabiti ndani ya Kristo. Damu ina Roho ya uhai ndani yake ambayo inapoingia au kuachiliwa mahali ghafla unaanza kuona ramani mpya ya maisha, picha mpya, uelekeo mpya na neno la Bwana la kukuvusha ambalo halitarudi bure. Jifunze kuachilia, kunyunyizia na kumwaga damu ya Yesu aliyehai juu ya msingi wa maisha yako, familia, ukoo na eneo ulilopo ili kubatilisha kila hila na makusudio yaliyo kinyume na haja ya moyo wako ndani ya Yesu na mapenzi ya Mungu aliye hai juu ya maisha yako ya baade.

03. 04 asili ya misingi (nature of foundation)

Kila kitu hata msingi una asili yake tokea rohoni, maana mambo yote asili yake ni rohoni ambavyo hudhihirishwa katika mwili (from spiritual nature into physical nature) ili viendelezwe kwa namna ya mwilini au katika ulimwengu wa mwili, yaani tokea visivyoonekana kuwa katika hali ya vinavyoonekana.  Kwa hiyo na masuala ya misingi yanaanzia katika ulimwengu wa roho.
Ulimwengu wa roho una pande mbili au unajumuisha falme zote mbili, yaani ufalme wa mbinguni, nuru yaani Mungu aliye hai na milki zake na malaika wake, pia ufalme wa giza yaani shetani na fahari zake na jeshi la pepo wabaya, wakuu wa anga na pepo wachafu. Kila ufalme una uwezo wa kuanzisha mfumo wa maisha au una uwezo wa kuathiri ulimwengu wa mwili kwa sababu kila ufalme una mamlaka, na nguvu ya kutawala na kumiliki japokuwa ufalme wa mbinguni yaani Mungu aliye hai au Yesu peke yake ndiye mwenye mamlaka kuu juu ya yote na ndani ya wote na juu ya vyote. Kwa hiyo, falme zote zinaweza zikaanzisha msingi wake, kama msingi ukianzishwa na ufalme wa Nuru basi ndio asili yake, na kama ukianzishwa na giza basi ndio asili yake.
Asili ya msingi unategemea na mwamba wa eneo, uwezo na nguvu ya mwenye kuujenga. Kwa hiyo tajiri au mwenye nguvu akijenga lazima atatumie gharama zaidi ili ajenge mwanzo au msingi mzuri ulio imara (yaani Kristo), lakini maskini anaweza kujenga na usidumu. Kiwango cha uimara wa msingi wa nguvu ya umiliki na utawala vinatengeneza kesho ya mtu aidha iliyo imara au mbovu hata wakati na vipindi au hali tofauti za mapito. Luka 6:48, Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri.

Misingi mingine imechimbwa chini sana kwa namna ambavyo si rahisi kuuchimbua kirahisi na kuuondoa wote hadi kuumaliza, mpaka nguvu ya ziada ya kutosha kuhakikisha unaondoa kila pando ambalo hakulipanda Mungu aliye hai katika Yesu Kristo. Ukielewa vizuri masuala ya misingi yaani uzito na mshiko wake ndipo unaweza kuingia gharama zaidi ili kubomoa na kung’oa msingi huo.
Maombi ya kuondoa, kung’oa, kuvunja, kuchimbua na kusafisha misingi ya maisha lazima yawe maombi ya kujitoa, kujidhabihu, ya gharama na muda mrefu ili kuachilia na kunyunyizia damu ya Yesu taratibu katika misingi yaani shina na mizizi yote kuikausha na kuondoa  ili kila kilichoshikiliwa kiwe huru au kiachiwe kwa ajili ya maisha ya baadae.
Sio misingi yote inabomolewa, kung’olewa na kuondolewa kirahisi au kwa mkupuo maana inategemea na uhalali, sababu za kuwepo, muda uliomaliza, uimara na asili yake hivo lazima uingie gharama fulani ya kukaa ndani ya kristo Yesu ili umpe nafasi ya kutenda kazi pamoja nawe sawa sawa na mapenzi yake katika eneo linaloshughulikiwa. Uimara na muda wa misingi unatofautiana, maana misingi mingine ilijengwa tangu vizazi, pia na gharama za kujengwa ni tofauti.
Mfano; mtu akizunguka kwa wachawi au waganga tofauti akitafuta msaada wa kumsaidia- labda wakati wa kuoa au wa kuolewa, uzao, kusoma, ugonjwa, ajira, au katika kesi mbalimbali ili ashinde labda kesi ya wizi, uuaji, ardhi n.k. Nguvu za giza zinafitinika ndani ya mtu huyo au familia kwa namna ambavyo zinatengeneza msingi imara au mzito au ukuta imara ili kumiliki na kutawala uzao ujao au maisha ya baadae yanaendelea kuwa ndani ya ufalme wa giza. Kuchomoka na kujinasua katika misingi ya namna hii lazima umwombe Kristo Yesu aingie na aketi pamoja nawe enzini pake ili uingie katika kazi ya faida. Misingi ya namna hii unaingia kwa kujifunika damu ya Yesu kwanza na kuanza kuachilia na kunyunyizia damu inayonena mema, ukombozi taratibu ili kuvunja misingi ya ufalme wa giza iliyosimikwa mahali.
KUMBUKA
Dhambi (yaani giza au giza ibilisi) inapoingia ndani ya mtu au familia haianzi kutawala kwanza bali inaanza kula na kutafuna kimya kimya, inatafuna ndani taratibu, kujenga na kuimarisha ufalme wake yaani kujenga ngome imara.
Kwahiyo wakati unaomba toba juu ya misingi, akilini mwako na katika ufahamu wako jua na tambua ya kuwa hauombi juu ya pepo moja au roho moja iliyokufanya utende dhambi, bali unaomba juu ya mfumo wa kiutawala wa ufalme ambao umeachilia roho iliyokufanya utende dhambi ili ufalme huo ujijulishe, ujitambulishe au ujidhihirishe uwepo wake.
Hivyo damu ya kifalme (Yesu aliyehai) inapoanza kuingia ndani inakuwa inaingia taratibu taratibu na kabla ya kufika ikulu ya ufalme, serikali au ngome ili kuziondoa, kuvunja, kuharibu na kuondoa uhalali wake, kuondoa mapando yote, mizizi, ngome na kila namna ya ugiza uliopo.
Mfano; Ukisoma kitabu cha Isaya 37; utaona mfalme wa Asharu alivyokuwa akijiinua, akijitapa na kumtukana Mungu wa Israeli, namna ambavyo alikuwa akitoa maneno ya kejeli, machafu na dharau kwa Mfalme Hezekia aliyekuwa akimtumikia Mungu aliye hai.
Mfalme Hezekia alipokereka na kuudhika kwa sababu ya kuinuliwa kwa miungu mingine aliamua kujifungia katika chumba cha siri ili kuomba kwa Mungu aliye hai, na Mungu alipomjibu alisema atafuatilia chanzo cha nguvu (misingi) inayompa kiburi mfalme wa Ashuru na kujiinua, hivyo atakausha maji ya mito yote iliyo ndani ya ardhi ili ardhi ya eneo hilo ikauke na kila kilicho hai katika ardhi hiyo kipoteze uhai, ilikuwa ni ishara katika ulimwengu wa roho wa Mungu wa Israeli kuachilia nguvu na uweza wake kwenye chanzo au chimuko la nguvu ya miungu ili kuifukuza na kuiondoa ndani ya eneo ilo.
Mungu anataka umkaribishe au umwite kwa njia ya maombi ili akaharibu nguvu ya adui mpaka  kule pa siri ilipojificha ili uwe huru katika maisha yako ndani ya Kristo Yesu.

 

03.05. Misingi hutengeneza mfumo fulani wa maisha ili uwe sehemu ya maisha ya mtu.


Inakufanya au inakujengea hali fulani kimaisha ambayo utakubaliana nayo, utaridhika nayo kuutumikia haijalishi mfumo au hali hyo ni mbaya au nzuri, unaipenda au hauipendi, uko tayari au la!
Mfano wa 01
Kut 3:7-8, Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.

Wana wa Israeli waliishi maisha ya mateso, manyanyaso, taabu, dhiki, shida na vilio vya kila siku walipokuwa utumwani Misri kwa kiwango cha miili yao kubadilishwa na  kufinyangwa mpaka yale mateso kuwa sehemu ya hali ya maisha yao ya kila siku, kuridhika nayo na kukubaliana nayo na kuutumikia mfumo wa namna iyo. Lakini licha ya kuteseka na kuumia sana cha ajabu au jambo la kushangaza, walipokombolewa na Mungu wao kwa mkono wa Musa kwa ishara na maajabu, bado walipokuwa njiani shida ndogo tu ilikuwa inawafanya wakumbuke utumwani, wanang¢ang¢ania kurudi Misri nchi ya mateso, taabu, dhiki, uonevu na vilio. Ni kitu gani kilikuwa kimewabana kwa kiwango hicho cha kutaka kurudi katika hali ngumu namna hiyo? Ni kwa sababu misingi ilikuwa imeshatengeneza mfumo wa utumwa, taabu, shida na mateso kwa kiwango cha kuridhika nayo, kuutumikia na kuuhishi hadi kuwa sehemu ya maisha yao

Mfano wa 02.
Luka 15:17-19, 21,  Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.

 Fikiria yule mwana mpotevu aliyevuruga mali aliyopewa na baba yake kama sehemu ya urithi kwa ajili maisha yake ya baadae alipoitumia vibaya kwa anasa za dunia na mwishowe kurudi nyumbani, kama angetaka kurudi kula pamoja na mataifa pamoja na  nguruwe ingemaanisha nini hiyo hali au ingeashiria nini? Maana yake kama mwana mpotevu angetamani kurudi tena ili ale chakula pamoja na nguruwe au mataifa ujue hali hiyo imeshajengeka ndani yake au ameshafinyangwa na kuwa sehemu ya mfumo huo au ufalme huo wa mateso, dhambi au mahangaiko hadi kukubaliana nayo, kuridhika nayo na kuwa sehemu ya maisha yake, na kuutumikia. Mwili wake umeshageuzwa asili yake, umefinyangwa na kubadilishwa na kuwa mfumo wa kuishi au hali ya kusihi katika maisha yake. Haoni tena utumwa, dhambi, mateso, magonjwa, taabu na mahangaiko, maana yake anaona hiyo ndiyo kawaida ya kuishi na yuko kawaida kabisa na maisha ya namna hiyo. Haleluya!! Haleluya!!, mtu wa Mungu.
Kuna namna ambavyo watu wengi waliookoka hawaoni faida ya maisha ya wokovu, kuishi maisha na matendo ya wokovu kiasi cha kutamani kurudi walikotoka, au kuendelea kula mavi ya zamani sababu misingi ambayo walikuwemo bado imewashikiria, imewakamatilia na iliumbika au ilijijenga ndani yao licha kwamba wamempokea Kristo lakini bado msingi wa maisha yao uko vilevile kama wa zamani yaani msingi wa giza, ili kutotamani kurudi kula tena mavi ya zamani au kutoyarudia matendo ya zamani, kwaiyo lazima kuoshwa ndani ya damu ya Yesu ili kubadilishwa nia na dhamili za ndani, pia kuamishiwa katika msingi mpya ndani ya Kristo Yesu.
Mfano 03
Mithari 3:1, Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Kanisa kutembea katika hali ya mazoea; Mungu hulisha kanisa kulingana na wakati, uhitaji wa  roho za watu wake, hali iliyoko, msimu na majira. Kwa hiyo ni jukumu la waliopewa madhabahu kunyenyekea mbele za Mungu kila wakati ili kuuliza ni chakula gani Mungu anataka kuachilia kwa muda fulani ili kulisha kondoo, kusaidia, kuokoa, kuponya na kuhuisha roho na nafsi za kondoo wake, na sio kufuata kanuni na taratibu za kibinadamu, kikanisa au kidini juu ya namna fulani kutoa chakula au kulisha  kondoo.
Kila wakati una vitu vyake na changamoto zake, njia za kupita, namna ya kupita, na upako wa kustahimili na kuvuka ambavyo viko kwa Mungu peke yake, siyo kwa wanadamu. Kanisa lingine linampa Mungu nafasi yake, heshima na utukufu lakini lingine hupanga , huandaa na kufundisha wanachoona wao kuwa ni chema ili kanisa lao likue kwa kadiri ya jitihada na mipango yao.
Misingi yote ni mizuri lakini Yesu mwenye chakula na kanisa akipewa nafasi anayostahili kupewa ndani ya kanisa au madhabahuni ni faida sana. Chakula kinachoachilia toka jikoni inategemea na walioko wana nini au nia gani mioyoni mwao juu ya ufalme wa mbinguni. Biblia inasema kuweni na nia hiyo hiyo kama aliyokuwa nayo Kristo.
Kanisa liko ili kueneza ufalme wa mbinguni, habari njema, kumtangaza Yesu kama kipaumbele nambari moja, lakini vipaumbele vya kanisa vimekuwa tofauti sana maana wanaangalia na kujitahidi kufanya vinavyoonekana na vinavyoharibika.
Kwa hiyo kutubu juu ya misingi kwa kuachilia damu ya Yesu kunafuta na kuondoa hali ya mazoea au mifumo fulani ambayo inamnyima Mungu aliye hai nafasi yake kama mmiliki na mtawala wa mfumo ili kuokoa, kuponya, kuendeleza na kugusa hali ya maisha ya watu wake, kwa kuwapa chakula au ujumbe anaotaka yeye mwenyewe Mungu aliye hai kuwapa (Ufu 2:16). Haleluya! Haleluya!  mtu wa Mungu.

03. 06. Unatoa mwelekeo wa maisha ya baadae aidha ya mtu, familia, ukoo, taasisi au eneo.


Misingi ni mwanzo ulioanzishwa ili uwe mwendelezo wa kitu kilichokusudiwa. Msingi uliowekwa kwa njia ya agano, sadaka, laana, au kiapo inakuwa na lengo la kufuatilizia jambo fulani au hali fulani ya baadae, mwanzo wa mfumo au hali fulani ili kuendeleza, kusimamia au kuruhusu mwendelezo kwa kadiri ya utaratibu, kanuni, miiko, mipaka au makubaliano/masharti yaliyowekwa katika kuamuru na kuendesha mfumo husika wa maisha aidha juu ya mtu, familia, ukoo, kanisa eneo n.k. Ayubu 30:4,6, Hung'oa mboga ya chumvi kwenye kichaka; Na mizizi ya mretemu ni chakula chao. Lazima hukaa katika mianya ya mabonde, katika mashimo ya nchi na ya majabali.

Kwanini Mungu aliye hai aliziumba mbingu na nchi? Na kwanini adui shetani alitafuta mahali ambapo Mungu alipaanzisha? Kwanini shetani hakutafuta mahali pengine?, Je! Ni kweli hali ya familia, ukoo au kanisa kwa sasa ni njema? Au la! Na kama sio, kitu gani kiliingia hapo katikati au njiani kikaharibu hali iliyokuwepo na mwendelezo wake?
Msingi unakutengenezea mazingira ya kukubana, kukunyima na kukutumikisha na kuachilia kiwango fulani cha uhuru wa maisha ya mtu katika kupiga hatua za kimaisha. Ayubu 38: 19),  Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi?

Maana yake huwezi kupiga hatua zaidi ya msingi inayokuamuru uhuru wa maisha yako, huwezi kuvuka wigo, kuta, pazia au uzio zilizokuzunguka mpaka zimevunjwa kwanza (Yeriko) ndio uweze kuvuka, kuona ngambo, kuangaza, kuchanua na kwenda mbele zaidi katika mfumo husika au hali ya maisha yako. Zab 4:6, Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema? Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.

Mungu ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, kwa hiyo kama yeye ni mwanzo na mwisho, anajua pa kuanzia na namna ya kuanza na pa kuishia, na Mungu hawezi kutuacha tuteseke, anatoa Nuru ya kutuongoza kule. Yohana 1:4-9Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu.


No comments:

Post a Comment