Friday, May 5, 2017

MISINGI NI NINI?!!!

MAANA YA MISINGI

Na 
Mosses Benedict
Mawasiliano +255 762 371 383
Karibuni katika madhabahu hii ya neno la Mungu aliyehai katika Kristo Yesu. Leo tutaangalia kwa pamoja maana ya Misingi katika maisha ya mwanadamu. Tutaona pia mifano mbalimbali inavyoelezea maana ya misingi katika maisha yetu.  
Endelea pamoja nami...........

Misingi; ni nafasi iliyoko katika ulimwengu wa roho, ambayo imeanzishwa, imejengwa au imetengenezwa ili iamuru, itawale na imiliki mifumo ya maisha ya watu tangu kuwekwa kwake na kuendelea au na baadae.
Inaweza ikawa katika ngazi tofautitofauti, mfano ngazi ya familia, ukoo, eneo, taasisi, nchi na mtu binafsi.
Inaweza kutawala mfumo mmojawapo wa maisha au mifumo yote ya maisha katika ngazi tajwa hapo juu.
Msingi; ni mwazo, chimbuko au kiini cha kitu, mtu, familia, kanisa, eneo au nchi au mfumo wa maisha ulioanzishwa au uliojengwa ili uwe mwendelezo wa kitu au mfumo wa maisha uliokusudiwa.
Maana yake kila linalofanyika linakuwa ndani ya kusudi lililokusudiwa au lililolengwa tangu mwanzo.
Msingi, kwa kawaida fikiria msingi wa nyumba, au msingi wa elimu (elimu ya msingi).
Mtu alivyo leo ni matokeo ya alivyojengwa, alivyofinyangwa au alivyoandaliwa, kwa hiyo kama mwazo ulikuwa mzuri au mbovu vivyo ivyo na kesho ya mtu itakuwa sawasawa na mwazoni palivyokuwa.
Takribani kabila na jamii zote za Afrika zilikuwa zinaabudu miungu tofautitofauti kabla ya ujio wa wamisionari kuleta dini/injili/habari njema/Nuru. Kwa hiyo misingi ya maisha au ibada ilikuwa imejengwa katika giza.
Misingi ni kama kisima ambako maji yanachimbuka au yanatokea. Kisima kinaweza  kutoa maji masafi au machafu, masafi ni uhai lakini machafu yanadhuru yanaleta magonjwa. Kwa hiyo ukitaka kusafisha maji ni lazma umimine damu ya Yesu ili kila anywaye apate uzima, aingie apate uponyaji. Kijito cha uzima kwa ajili ya maisha ya baadae.(Yeremia 6:7-8)
Mungu anasema tumuulize juu ya mapito au njia za zamani au ya mwazoni (msingi) au tuwaulize waliokuwepo wanazifahamu njia sahihi ili tupate kujua huko nyuma hali ya maisha ilikuwaje.(Ayubu 8:4-10)
Kwanini tulihama au tulipotea ili turudi katika njia sahihi na njema kwa ajili ya maisha ya baadae? (Yeremia 6:16)
Tupate mifano kadhaa ambayo inaweza kueleza zaidi hali ya mwazo wa maisha (misingi) ambayo inaweza kuharibiwa, kuchafuliwa au kuingilia na kupelekea hali ya maisha ya mtu, jamii, familia, ukoo, kanisa au nchi kubadilika hali yake kimaisha. (Ezra 3:10-12)
Mfano 01
Ukisoma kitabu cha Ezra 3:12-13, utaona namna ambavyo wana wa Israeli walitoa sadaka, na hiyo fedha walipewa waashi au wajenzi. Wajenzi walipoanza kujenga au kuweka /kusimanisha msingi wa nyumba ya Mungu wa Israeli, utaona Makuhani na Walawi wakiwa wamevaa mavazi yao wanaanza kumhimidi Bwana na kumwimbia na kumshukuru, pia utaona wazee waliokuwepo zamani walioona nyumba ya Mungu ya mwazoni kabla ya kuharibika wanaanza kupiga kelele kwa sauti za furaha.
Kuna namna fulani ambavyo kujengwa kwa msingi wa nyumba ya Mungu wao kulikuwa kunagusa hali yao ya maisha wanayoishi. Mungu hakuwa na mahali pa kuishi au kukaa katikati yao, kwahiyo kujenga msingi wa nyumba ya Mungu wa Israeli ilikuwa ni ishara katika ulimwengu wa roho ya kuruhusu tena au kuita au  kumkaribisha Mungu wa Israeli katikati yao au miongoni mwao.
Watu walipiga kelele na kushangilia kwa furaha na kulia sio kwa sababu ya misingi inayoonekana kwa macho ila nguvu ya Mungu wao, utukufu ambao ulirejea, uriwarudia katika kuishi kwao ambako, Mungu kuwepo mahali anatawala na kumiliki hali ya maisha ya watu katika kila mfumo wa maisha yao.
Kwahiyo, toba juu ya misingi iliyoharibika, iliyokufa ni kwa ajili ya kurudisha heshima kwa Mungu, utukufu wake na nguvu zake ili kumiliki na kutawala hali ya maisha ya ngazi zote zinazochimbuka katika aridhi aliyokaribishwa.
Mfano 02
Mungu alipomuumba Adamu alimpa mamlaka na nguvu (authority and power) itakayotumika katika kutawala na kumiliki eneo, ardhi na mbingu zilizo juu ya eneo alilopewa. Kwa hiyo wakati huo hali ya maisha ya Adamu ilikuwa imefunikwa na wingu na roho yake vilivyokuwepo kwa namna ambavyo kila hali, kuishi, mifumo ya maisha, shughuli na tabia ilikuwa ndani ya nguvu au utukufu wa Mungu.
Baada ya maisha ya Adamu kutenda dhambi, kuasi au kutengwa Na uso wa Mungu wake, Adamu alibaki kuwa mtu wa Mungu lakini, Mungu aliondoa mamlaka aliyokuwa amempa nguvu zake, utukufu na roho yake ya kiutendaji. Kwa hiyo nguvu ya kumiliki na kutawala mifumo ya maisha au hali ya maisha iliondolewa  hivyo hali ya maisha na mwendelezo wa maisha ya Adamu haukuwa chini Mungu tena, bali chini ya uongozi wa Adamu nwenyewe na nguvu ya uasi, giza au adui akaanza kutawala na kumiliki hali na mifumo yote  ya maisha.
Kwahiyo kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni na kwa  njia moja uzima uliletwa ulimwenguni, ujio wa Yesu ulikuwa ni kurudisha utawala na umiliki wa ufalme wa mbinguni, mamlaka, nguvu, heshima ya Mungu na nafasi yake katikati  ya watu walioko ulimwenguni ambayo ilikuwa imeondolewa.
Hivvo, Yesu hakuja kama Yesu tu bali alikuja ili kurudisha, kurejesha mamlaka ya kiutawala, umiliki wake, utukufu wa Mungu aliye hai na ufalme wa mbinguni ili kuondoa ufalme wa giza uliokuwa ukitawala.
Kwa hiyo ujio waYesu mwenye nyota za kifalme mabegani mwake, aliyejaa neema na kweli ni ili kurudisha utawala, umiliki, heshima, utukufu, nguvu kwa ajili ya maisha ya watu kuwa kama mwazo kabla ya dhambi.
Hivyo tunapoomba toba katika misingi kwa kuachilia damu ya Yesu kwa jina lake juu ya misingi maana yake tunakuwa tunaandikisha utawala wake, ufalme, nguvu, utukufu heshima na nafasi yake ya kutawala na kumiliki ili maisha yetu yawe kama hali ya mwanzo, iliyo chini ya uongozi wa Mungu aliyehai.
Mfano 03
Ukisoma kitabu cha 2 Wafalme:18 utagundua kuwa kuna namna fulani ambayo Mungu wa Israeli aliyetakiwa kumiliki na kutawala hali ya maisha ya watu na eneo kipindi cha uongozi wa mfalme Ahabu, bali roho za Mungu zilizokuwa ndani ya mkwewe Yezebeli.
Eliya  alipotaka kurudisha utawala na umiliki wa Mungu wa Israeli ilimbidi na ilimgharimu atengeneze mahali palipobomoka au palipoharibika  (madhabahu iliyovunjika) (2 wafalme 18:30) ili kumtengenezea Mungu mazingira/sehemu/eneo au mahali pa kushuka, kukaa na kuachilia nguvu zake, utukufu , utawala  na roho ya utendaji ya kuthihirisha uwepo wake.
Eliya alitaka ijulikane katika wote na pote kuwa Mungu wa Israel, Ibrahimu, Isaka na Yakobo ndiye Mungu peke yake, maana yake ndiye mtawala na mmiliki, mwenye kujidhihirisha katika utukufu wake, nguvu zake na roho yake ya utendaji, hakuna miungu, nguvu na utawala mwingine ila yeye peke yake.
Eliya alimwita mfalme, mtawala, mmiliki, mwenye utawala na umiliki kwa mamlaka yake na nguvu zake ili ajidhihirishe katika utukufu wake, naye Mungu wa Israeli alijidhihirisha kwa kujibu kwa moto, ishara ya kuonesha roho yake ya utendaji iko kazi unapoikaribia ili ifanye kazi yake mahali fulani.
Kwa hiyo tunaomba toba katika misingi iliyoharibika, eneo, uongozi, familia, ukoo, kanisa, kwa kunyunyiza na kumwaga damu ya Yesu ni ili roho ya uhani iliyoko ndani ya damu ya Yesu kutenda kazi, na kuachilia uhai mpya, nguvu iliyo ndani ya damu, na mfalme (Mungu aliye hai) anashuka kuja kutawala na kumiliki juu ya eneo, kanisa, familia, au mfumo ambako toba imefanyika au inalenga. Lengo ni Mungu kutawala na kumiliki tena kama mwanzo, kupewa heshima na nafasi yake kama mfalme, mtawala na mmiliki halali. 
Misingi inaamuru masuala au hali mbalimbali au inashughulika na hali mbali mbali za maisha kama vile:
  • Nafasi fulani za uzao katika familia au ukoo kufariki, mfano; watoto wa kwanza au wa mwisho.
  • Kutovuka hatua kielimu, au kusoma na kuendelea bila kufanikiwa na anayechomoka tu, kufariki.
  • Kufungiwa ndani ya eneo, kubanwa ndani ya eneo.
  • Kutooa au kutoolewa, kuachika au kutengana, pia kuzaa kabla ya ndoa rasmi.
  • Kuanzisha kitu (biashara) na kuishia njiani, mfano; biashara mara ghafla mtu anafunikwa na giza na kupoteza fikra, wazo au msukumo aliokuwa nao kuisha ndani yake.
  • Utengano, mafarakano, maneno kati ya ndugu, mke na mume, kanisa, kwaya, vikundi vikundi ndani ya familia, kanisa au eneo fulani
ITAENDELEA...............
Asante kwa kuwa nami.
Mshirikishe na mwenzako ili apate nae huduma hii.
 Waweza kutoa maoni, ushauri, au mapendekezo yatakayosaidia kukuza na kuendeleza madhabahu hii, katika kisanduku hapa chini.

2 comments:

  1. Huu Ni Upotosha Mkubwa wa Neno la Mungu. Hiyo siyo Maana Halisi ya Neno Misingi kwa Mujibu wa Maandiko Matakatifu. Ukweli wa Neno Misingi Una- Maana Ifuatayo ktk Vitabu Vitakatifu: Tizama Misingi ya Mungu ktk Agano la Kale Na Agano Jipya:- (i) Agano la Kale= Kutoka 20:1-17 Na Agano Jipya Ni = Wagalatia 5:18-21. Hiyo Ndiyo Misingi ya Mungu Amabayo Wakristo wote Tumejengwa Juu yake. Kama Maandiko yanavyotamka :- Tumejengwa juu ya Msingi wa Mitume Na Manabii:- Waefeso 2:19-22. Karibu tuendelee Kumtafuta Mungu aliye kweli yote.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom. Tafsiri ya kwanza na ya pili ni sawa maana kila mtu huwa ànapata ufunuo wake. Asante

      Delete