Friday, May 5, 2017

VITU MUHIMU VYA KUJUA KATIKA MASUALA YA MISINGI


Na Mosses Benedict
Mawasiliano +255 762 371 383
Siku chache zilizopita tuliona maana halisi ya misingi. Tuliangalia pia mifano kadhaa inayotuonesha maana ya misingi. 
Katika somo la leo, tutaangalia vitu muhimu katika masuala ya misingi. Kwa kusoma makala hii, tutabarikiwa sana, hali kadhalika tutakuwa na uelewa wa mambo muhimu sita (06), katika masuala ya misingi pamoja na mifano yake

Endelea nami.......................

01. Uhalali wa misingi
Misingi inaweza kuwa halali au ya uonevu; Biblia inasema tulikuwepo kabla ya kuumbwa kwa misingi ya dunia hii hivyo Mungu alipotaka kuleta ufalme wake hapa duniani, au alipoamua kutanua na kupanua ufalme wake wa mbinguni ili kuudhihirisha kwa namna ya kimwili alitengeneza mazingira kwanza (misingi) ambayo ufalme wake utafikia na utaanzia kama mwanzo wa maisha au kama msingi wa maisha ya watu wake.

Mwanzo wa kuanzia ambako kulikuwa na utukufu wake, Uungu, uweza, umiliki na utawala wake au uzima katika yote ili uwe mwendelezo wa maisha ya baadae tokea katika msingi huo. Lakini dhambi iliingia katika msingi huo (Edeni) na kuanza kuachilia na kuzaa vitu tofauti (mauti) na vilivyokusudiwa tangu mwanzo (uzima) (Rum 5:12).

Misingi inapata uhalali kwa kujengwa, au kusimikwa au kuwekwa rasmi wahusika tofauti kama; wakuu wa ukoo au familia, wakuu wa dini, eneo au nchi, viongozi juu ya eneo wanayotawala, ndugu. Wahusika hawa wanaweza kusimika au kuweka uhalali wa misingi kwa njia mbalimbali kama vile; sadaka, agano, kiapo, laana na kujenga mfumo wa maisha unaogusa vizazi au uzao wa baadae na hali yao ya maisha.

Mfano wa 01

Ibrahimu aliingia katika agano na Mungu aliye hai, mwanzo yeye kama baba wa familia yake na ulimwengu mzima. Sadaka yake na maisha ya familia yake na ulimwengu mzima. Pia agano alilolitunga na Mungu aliye hai liligusa maisha ya familia yake kwa ujumla na ulimwengu wote, kabila na mataifa katika agano jipya, yaani kwa yesu Kristo. Maana yake Ibrahimu alikuwa na nafasi ya kutengeneza mazingira ya aidha kubarikiwa, au kinyume juu ya familia yake nzima na ulimwengu wote. Msingi au mwanzo au chimbuko la Baraka.

Mfano wa 02

Kuna baba mmoja ambaye aliamua kufanya biashara ya mbao katika msitu wa Mpanda- Rukwa. Ili uingie katika msitu huo, ufanye kazi zako vizuri na ufanikiwe kulikuwa na kanuni na taratibu za mila na desturi za mahali pale ambapo ilibidi uwaone wazee wa eneo lile ili wakueleze yakupasayo. Baba huyo aliingia katika kutekeleza taratibu na kanuni zao kwa kutoa sadaka na kiapo ambacho kilihusisha familia yake na mifumo ya maisha yao yote. Baada ya muda mke wake alianza kuugua magonjwa ya ajabu ambayo kila akienda na kupima hospitali hawaoni tatizo, alikuwa anahisi mwili unawaka moto, miguu kama vile anakanyaga juu ya misumari inamchoma mpaka anashindwa kutoka ndani, anaumwa mgongo kila siku. Watoto wote walianza kuugua magonjwa ya ajabu mara kuishiwa maji mwilini, upofu, pia kielimu wote walikuwa wanashindwa licha ya kupelekwa katika shule kubwa zenye mazingira mazuri ya watoto kushinda lakini walikuwa wakirudia rudia. Mtoto wa mwisho alikuwa kama taahira hivi, ambako alifika darasa la sita akiwa hajui kusoma na kuandika vizuri lakini ana uwezo wa kutaja wachezaji wa timu za mpira za hapa Tanzania na wachezaji wa ulaya bila kukosea.

Baba aliingia agano na viapo vilivyomgusa yeye binafsi, familia nzima na mifumo ya maisha yao yote. Ili wawe huru ni lazima kuachilia, kunyunyizia na kumwaga damu ya Yesu katika msingi ili kufuta uhalali wake alioupata kwa njia ya sadaka, viapo na maagano. Damu ya Yesu inalipa gharama ya sadaka hiyo, inavunja maagano na viapo ili familia na maisha yao yawe huru ndani ya Kriso Yesu kwa njia ya damu yake Yesu Kristo.

Sadaka itanena juu ya wote walio ndani ya familia hiyo, ukoo, kanisa, eneo au himaya husika. Agano linagusa, linatungamanisha au ndani yake linabeba au linatawala maisha ya uzao wa aliyelifanya au aliyeanzisgha msingi huo wa kiagano. Laana inafuatilia tokea kizazi husika mpaka vijavyo na kuachilia vitu vilivyobebwa ndani yake ili kuwapa walio ndani ua msingi huo kilaana. Na kiapo kinamfunga yeye aliyeapa na wote walio chini yake, katika tawala au umiliki wake.

Huwezi kuondoa uhalali wa misingi pasipo kibali, agizo au uhalali. Misingi iwe halali kwamba ilisimikwa na watu au iwe ya uonevu tu wa adui shetani, zote zinafutiwa uhalali wake na kuondolewa kabisa kwa njia ya damu ya Yesu aliye hai ili kutengeneza msingi mpya ulio bora ndani ya Kristo Yesu.

02. Sababu za kuwepo kwa misingi (motives of reasons behind)

Sababu zinazopelekea kuanzishwa au kuwekwa kwa misingi fulani zinatofautiana. Inawezekana misingi inalenga mtu binafsi, jinsia, familia nzima, ukoo mzima, eneo la kiongozi kulingana na ngazi husika, wanafunzi fulani au wote ndani ya mipaka ya shule au chuo, kondoo au waumini walio chini ya mtumishi fulani, mfumo mmojawapo (au mifumo yote ya maisha) ambao ukiguswa na mifumo mingine itaguswa moja kwa moja au siyo moja kwa moja.

Inawezekana msingi uliosimikwa ulikusudiwa ufanye kazi kwa kipindi fulani, majira au wakati fulani.

Mfano; kwa ngazi ya familia au ukoo, mtu akifikia hatua/umri wa kuoa au kuolewa, mtu anapochanua kiuchumi aidha afe, awehuke au afilisike, mtu akiingia katika ngazi fulani ya kielimu, kufariki kwa nafasi fulani ya uzao ndani ya familia au ukoo labda kila mtoto wa kwanza au mtu fulani akifa vitu fulani ndio vianze kulipuka au kufanya kazi au ndio vianze kuonekana, mtu anapookoka au kuanza kumtumikia Mungu ndio upinzani na vita vinapoanza na kuinuka juu yake kukataliwa na ndugu, walezi , kanisa na waumini.

Msingi unaanzishwa au unajengwa ili uwe mwendelezo (urithi) mpaka ghafla kuingilie nguvu ya kuvunja huo mnyororo (chain), kuharibu na kung¢oa msingi huo ili vilivyokuwa vimekamatiliwa ndani yake viwe huru (Yer 1:9-10)

03. Malengo ya msingi

    Kusudi la kujenga msingi mbele yako, wanaweka nini wanapoujenga leo kwa ajili ya maisha yako ya baadae? Sababu za kusimamisha msingi mbele yako zipo kadhaa kama:

    Kukuzungushia wigo ili ukitaka kuvuka ukutane na ukuta (mipaka ili usivuke) yaani vizuizi, vikwazo katika eneo fulani ili uzunguke humo humo kimaisha na kihuduma.

    Lengo la kukuwekea ukuta mbele, wigo au uzio ni usione mbele, uone giza tu, ukate tamaa, urudi nyuma ujione huwezi, hufai, huna maana.

    Ukuta; ni kuziba mahali unapotakiwa upaone ili usipaone au unapotakiwa kwenda au kuvuka ili usivuke. Lengo ni uishi au ukae ndani ya eneo hilo hilo au mfumo huo huo ili uendelee kuona yale yale kama kuonewa, kudharauliwa ugumu n.k.

Kukutafakarisha au kukufikirisha yaliyo ndani ya msingi uliomo, ufahamu, akili, fikra, na kuamini hujengwa katika vitu unavyoona, unavyosikia na unavyoishi.

Mfano; ukiishi katika familia au ukoo uliozungukwa na vifo, magonjwa, kutooa, au kuolewa, ulevi, kuabudu miungu, na kutopiga hatua kimaisha aidha kielimu au kiuchumi, lazima huwezi kuona sababu ya kukusukuma kuvuka au kutoona sababu ya kutokutofautisha na mfumo wa maisha uliokuzunguka na wengine wanaokuzunguka. Mpaka neema ya Mungu aliye hai au uone nuru ya kukusaidia kuona mbali, kuona tofauti na hali ilivyo.

Kukujengea mfumo uliopofushwa ndani yako ili uone na useme kulingana na upofu ulio nao au uliotiwa ndani yake. Maamuzi yanayosukumwa na unavyoona, unavyosikia, unavyofikiri au unavyotafakari kwa kuangalia hali au changamoto zilizopo bila kujua zimeletwa na nini au chanzo chake ni nini au chimuko, kiini ili ushughulike na chanzo au msingi wa tatizo (2Kor 4:3).

Kwa hiyo kazi ya damu ya Yesu inaponyunyiziwa katika misingi inabadilisha na kubatilisha malengo ya misingi ya giza kama wigo na kuta zinayeyushwa mbele yake, utatafakarishwa na uhai uliomo ndani ya damu ya Yesu, kujengewa msimamo dhabiti ndani ya Kristo. Damu ina roho ya uhai ambayo inapoingia au kuachiliwa mahali ghafla unaanza kuona ramani mpya ya maisha, picha mpya, uelekeo mpya na neno la Bwana la kukuvusha ambalo halitarudi bure. Jifunze kuachilia, kunyunyizia na kumwaga damu ya Yesu juu ya msingi wa maisha yako, familia, ukoo na eneo ulilopo ili kubatilisha kila hila na makusudio yaliyo kinyume na haja ya moyo wako ndani ya Yesu na mapenzi ya Mungu aliye hai juu ya maisha yako ya baade.

04. Asili ya misingi (nature)

Kila kitu hata misingi ina asili yake tokea rohoni, maana mambo yote asili yake ni rohoni ambavyo hudhihirishwa katika mwili (physical nature) ili viendelezwe kwa namna ya mwilini au katika ulimwengu wa mwili, tokea visivyoonekana kuwa katika hali ya vinavyoonekana.  Kwa hiyo na masuala ya misingi yanaanzia katika ulimwengu wa roho.

Ulimwengu wara roho una pande mbili au unajumuisha falme zote mbili, yaani ufalmewa mbinguni, nuru (Mungu aliye hai) na milki zake na malaika wake, pia ufalme wa giza (shetani). Kila ufalme una uwezo wa kuanzisha mfumo wa maisha au una uwezo wa kuathiri ulimwengu wa mwili kwa sababu kila ufalme una mamlaka, na nguvu ya kutawala na kumiliki japokuwa ufalme wa mbinguni, Mungu aliye hai au Yesu peke yake ndiye mwenye mamlaka kuu juu yote na ndani ya wote.

Kwa hiyo, falme zote zinaweza zikaanzisha msingi wake. Kama msingi ukianzishwa na ufalme wa nuru basi ndio asili yake, na kama ukianzishwa na giza basi ndio asili yake.

Asili ya msingi unategemea na mwamba wa eneo, uwezo na nguvu ya mwenye kuujenga. Kwa hiyo tajiri au mwenye nguvu akijenga lazima atumie gharama zaidi ili ajenge mwanzo mzuri ulio imara (Kristo), lakini maskini anaweza kujenga na usidumu. Kiwango cha uimara wa msingi wa nguvu ya umiliki na utawala vinatengeneza kesho ya mtu, aidha iliyo imara au mbovu hata wakati na vipindi au hali tofauti za mapito (Lk 6:48).

Misingi mingine imechimbwa chini sana kwa namna ambavyo si rahisi kuuchimbua kirahisi na kuuondoa wote hadi kuumaliza, mpaka nguvu ya ziada ya kutosha kuhakikisha unaondoa kila pando ambalo hakulipanda Mungu aliye hai katika Yesu Kristo.

Ukielewa vizuri masuala ya misingi yaani uzito na mshiko wake ndipo unaweza kuingia gharama zaidi ili kubomoa na kung’oa msingi huo.

Maombi ya kuondoa, kung’oa kuvunja, kuchimbua na kusafisha misingi ya maisha lazima yawe maombi ya kujitoa, kujidhabihu, ya gharama na muda mrefu ili kuachilia na kunyunyizia damu ya Yesu taratibu katika misingi yaani shina na mizizi yote kuikausha na kuondoa  ili kila kilichoshikiliwa kiwe huru au kiachiwe kwa ajili ya maisha ya baadae.

Sio misingi yote inabomolewa, kung’olewa na kuondolewa kirahisi au kwa mkupuo maana inategemea na uhalali, sababu za kuwepo, muda uliomaliza, uimara na asili yake hivo lazima uingie gharama fulani ya kukaa ndani ya kristo Yesu ili umpe nafasi ya kutenda kazi pamoja nawe sawa sawa na mapenzi yake katika eneo linaloshughulikiwa.

Uimara na muda wa misingi unatofautiana, maana misingi mingine ilijengwa tangu vizazi, pia na gharama za kujengwa ni tofauti.

Mfano; mtu akizunguka kwa wachawi au waganga tofauti akitafuta msaada wa kumsaidia- labda wakati wa kuoa au wa kuolewa, uzao, kusoma, ugonjwa, ajira, au katika kesi mbalimbali ili ashinde labda kesi ya wizi, uuaji, ardhi n.k. Nguvu za giza zinatiririka ndani ya mtu huyo au familia kwa namna ambavyo zimetengeneza msingi mzito au ukuta imara ili kumiliki na kutawala uzao ujao au maisha ya baadae yanaendelea kuwa ndani ya ufalme wa giza. Kuchomoka na kujinasua katika misingi ya namna hii lazima umwombe Kristo Yesu aingie na aketi pamoja nawe enzini pake ili uingie katika kazi ya faida.

Misingi ya namna hii unaingia kwa kujifunika damu ya Yesu kwanza, na kuanza kuachilia na kunyunyizia damu inayonena mema ukombozi taratibu ili kuvunja misingi ya ufalme wa giza iliyosimikwa mahali.

KUMBUKA
Dhambi au giza (ibilisi) inapoingia ndani ya mtu au familia haianzi kutawala kwanza bali inaanza kula na kutafuna kimya kimya, inatafuna ndani taratibu, kujenga na kuimarisha ufalme wake yaani kujenga ngome imara.

Kwahiyo wakati unaomba toba juu ya misingi, akilini mwako na katika ufahamu wako jua na tambua ya kuwa hauombi juu ya pepo moja au roho moja iliyokufanya utende dhambi, bali ufalme huo ujijulishe, ujitambulishe au ujidhihirishe uwepo wake.

Hivyo damu ya kifalme (Yesu) inapoanza kuingia ndani inakuwa inaingia taratibu na kabla ya kufika ikulu ya ufalme, serikali au ngome ili kuziondoa, kuvunja, kuharibu na kuondoa uhalali wake, kuondoa mapando yote, mizizi, ngome na kila namna ya ugiza uliopo.

Mfano; Ukisoma kitabu cha Isaya 37; utaona mfalme wa Asharu alivyokuwa akijiinua, akijitapa na kumtukana Mungu wa Israeli, namna ambavyo alikuwa aitoa maneno ya kejeli, machafu na dharau kwa Mfalme Hezekia aliyekuwa akimtumikia Mungu aliye hai.

Mfalme alipokereka na kuudhika kwa sababu ya kuinuliwa kwa miungu aliamua kujifungia katika chumba cha siri kuomba kwa Mungu aliye hai, na Mungu alipomjibu alisema atafuatilia chanzo cha nguvu (misingi) inayompa kiburi na kujiinua, hivyo atakausha maji ya mito yote iliyo ndani ya ardhi ili ardhi ya eneo hilo ikauke na kila kilicho hai katika ardhi hiyo kipoteze uhai.

Mungu anataka umkaribishe au umwite kwa njia ya maombi ili akaharibu nguvu ya adui mpaka kule pa siri ilipojificha ili uwe huru katika maisha yako.

05.Misingi hutengeneza mfumo fulani wa maisha ili uwe sehemu ya maisha ya mtu.

Inakufanya au inakujengea hali fulani kimaisha ambayo utakubaliana nayo, utaridhika nayo kuutumikia haijalishi mfumo au hali hyo ni mbaya au nzuri, unaipenda au hauipendi, uko tayari au la!

Mfano wa 01

Wana wa Israeli waliishi maisha ya mateso, manyanyaso, taabu, dhiki na shida utumwani Misri na vilio vya kila siku, lakini miili yao ilikuwa imeshabadilishwa, imeshafinyangwa na yale mateso kuwa sehemu ya hali ya maisha yao ya kila siku, kuridhika nayo na kukubaliana nao na kuutumikia. Lakini licha ya kuteseka na kuumia sana cha ajabu au jambo la kushangaza, walipokombolewa na Mungu wao kwa mkono wa Musa kwa ishara na maajabu, lakini walipokuwa njiani shida tu ilikuwa inawafanya wakumbuke utumwani, wanang¢ang¢ania kurudi Misri nchi ya mateso, taabu, dhiki, uonevu na vilio. Ni kitu kilikuwa kimewabana kwa kiwango hicho cha kutaka kurudi katika hali ngumu namna hiyo? Kwa sababu misingi ilikuwa imeshatengeneza mfumo wa utumwa, taabu, shida na vilikuwa sehemu ya maisha yao (Kut 3:7-8).

Mfano wa 02

Fikiria yule mwana mpotevu alivuruga mali aliyopewa na kurudi nyumbani, kama angetaka kurudi kula pamoja na nguruwe, ingemaanisha nini hiyo hali au ingeashiria nini? Maana yake kama mwana mpotevu angetamani kurudi tena ili ale chakula na nguruwe au mataifa ujue hali hiyo imeshajengeka ndani yake au ameshafinyangwa na kuwa sehemu ya mfumo huo au ufalme huo wa mateso, dhambi au mahangaiko hadi kuukubali, kuridhika nao na kuwa sehemu ya maisha yake, na kuutumikia. Mwili wake umeshageuzwa asili yake, umefinyangwa na kubadilishwa na kuwa mfumo wa kuishi au hali ya kusihi katika maisha yake. Haoni tena utumwa, dhambi, mateso, magonjwa, taabu na mahangaiko. Maana yake anaona hiyo ndiyo kawaida ya kuishi na yuko kawaida kabisa na maisha ya namna hiyo. Haleluya!! Haleluya!!, mtu wa Mungu. (Lk 15:11).

Mfano 03

Kanisa kutembea katika hali ya mazoea; Mungu hulisha kanisa kulingana na wakati, uhitaji wa  roho za watu wake, hali iliyoko, msimu na wakati. Kwa hiyo ni jukumu la waliopewa madhabahu kunyenyekea mbele za Mungu ili kuuliza ni chakula gani Mungu anataka kuachilia kwa muda fulani ili kulisha na kuhuisha roho na nafsi za kondoo wake, na sio kufuata kanuni na namna fulani kutoa chakula kwa kondoo.

Kila wakati una vitu vyake na changamoto zake, na upako wa kustahimili na kuvuka ambavyo viko kwa Mungu peke yake, siyo kwa wanadamu.

Kanisa lingine linampa Mungu nafasi yake, heshima na utukufu lakini lingine hupanga, huandaa na kufundisha wanachoona wao kuwa ni chema ili kanisa lao likue kwa kadiri ya jitihada na mipango yao.

Misingi yote ni mizuri lakini Yesu mwenye chakula na kanisa akipewa nafasi anayostahili kupewa ndani ya kanisa au madhabahuni ni faida sana. Chakula kinachoachilia toka jikoni inategemea na walioko wana nini au nia gani mioyoni mwao juu ya ufalme wa mbinguni. Biblia inasema kuweni na nia hiyo hiyo kama aliyokuwa nayo Kristo (Mith 3:1).

Kanisa liko ili kueneza ufalme wa mbinguni, habari njema, kumtangaza Yesu kama kipaumbele nambari moja, lakini vipaumbele vya kanisa vimekuwa tofauti sana maana wanaangalia na kujitahidi kufanya vinavyoonekana na vinavyoharibika.

Kwa hiyo kutubu juu ya misingi kwa kuachilia damu ya Yesu kunafuta na kuondoa hali ya mazoea au mifumo fulani ambayo inamnyima Mungu aliye hai nafasi yake kama mmiliki na mtawala wa mfumo ili kuendeleza hali ya maisha ya watu wake, kwa kuwapa chakula au ujumbe anaotaka yeye mwenyewe Mungu aliye hai kuwapa (Ufu 2:16).

06. Unatoa mwelekeo wa maisha ya baadae aidha ya mtu, familia, ukoo, taasisi au eneo.

Misingi ni mwano, sadaka, laana, au kiapo inakuwa na lengo la kufuatilizia jambo fulani au hali Fulani. Mwanzo wzo ulioanzishwa ili uwe mwendelezo wa kitu kilichokusudiwa. Msingi uliowekwa kwa njia ya agana mfumo au hali fulani ili kuendeleza, kusimamia au kuruhusu mwendelezo kwa kadiri ya utaratibu, kanuni, miiko, mipaka au makubaliano/masharti yaliyowekwa katika kuamuru na kuendesha mfumo husika wa maisha aidha juu ya mtu, familia, ukoo, kanisa eneo n.k. (Ayubu 30:4,6).

Kwanini Mungu aliye haai aliziumba mbingu na nchi? Na kwanini adui shetani alitafuta mahali ambapo Mungu alipaanzisha?, Kwanini shetani hakutafuta mahali pengine?, Je! Ni kweli hali ya familia, ukoo au kanisa kwa sasa ni njema? Au la! Na kama sio, kitu gani kiliingia hapo katikati au njiani kikaharibu hali iliyokuwepo na mwendelezo wake?

Msingi unakutengenezea mazingira ya kukubana, kukunyima na kukutumikisha na kuachilia kiwango cha fulani cha uhuru wa maisha ya mtu katika kupiga hatua za kimaisha. (Ayubu 38: 19).

Maana yake huwezi kupiga hatua zaidi ya msingi inayokuamuru uhuru wa maisha yako, huwezi kuvuka wigo, kuta, pazia au uzio zilizokuzunguka mpaka zimevunjwa kwanza (Yeriko) ndio uweze kuvuka, kuona ngambo, kuangaza, kuchanua na kwenda mbele zaidi katika mfumo husika au hali ya maisha yako (Zab 4:6).

Mungu ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, kwa hiyo kama yeye ni mwanzo na mwisho, anajua pa kuanzia na namna ya kuanza na pa kuishia, na Mungu hawezi kutuacha tuteseke, anatoa nuru ya kutuongoza kule (Yn 1:4-9).

ASANTE SANA KWA KUSHIRIKI NAMI KATIKA MAKALA HII.
Wiki ijayo tutakuja na mada ya

Uweza na nguvu iliyomo ndani ya damu ya yesu juu ya misingi na inavyogusa hali ya maisha ya watu ya baadae"

Weka maoni, mapendekezo au ushauri wako, katika kusaidia kukuza na kuboresha madhabahu hii ya Bwana.

Ubarikiwe sana

No comments:

Post a Comment