Tuesday, May 30, 2017

NAMNA AMBAVYO MUNGU ANAWEZA KUJIBU TUNAPOFANYA MAOMBI YA TOBA KATIKA MISINGI

Na Mosses Benedicto 
 Mawasiliano +255 762 371 383
Tunapofanya maombi ya toba katika misingi kwa kuachilia na kunyunyizia au kumwaga damu ya Yesu, kumbuka jambo hili muhimu, kuwa tunakuwa tunaachilia Roho ya Mungu itendayo kazi iliyo ndani ya damu ya mwana wake, kwa hiyo Roho wa Mungu anashuka na kuanza kufanya kazi (operation) katika eneo lolote ambalo mwana wa ufalme ameachiwa.

Roho hiyo inatenda kazi kwa namna au njia tofauti tofauti ambazo tunaweza kusema ni namna ya Mungu aliyehai kutenda kazi yake katika Roho yake, hivyo zifuatazo ni baadhi ya njia au namna ambavyo Mungu aliyehai anajibu ikiwa watu wake wameomba toba katika misingi au wamemkaribisha. Mungu anaweza kujibu au kujidhiirisha kwa namna tofauti tofauti unapomkaribisha juu ya misingi, baadhi ni izi zifuatazo;

05. 01.  Kutetemesha misingi

Zabri 18:7, Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Mungu aliyehai anaweza kuachilia nguvu ya tetemeko ili kutetemesha eneo zima ambalo misingi ya nguvu za adui zimesimikwa, zimejengwa au zimesimamishwa; eneo au ardhi ambayo misingi na mizizi yake  na nguvu zake inapotetemesha kuna mizizi, kamba, nyuzi, tanzi na vifungo ambavyo vinaanza kukatika taratibu kadiri ya nguvu ya Mungu inavyozidi kuachiliwa, kwa hiyo Roho wa Mungu anapoachiliwa juu ya misingi ya adui, kazi mojawapo anayoifanya ni kutetemesha misingi ili nguvu za adui na vifungo viachie, vikatike na kuvunjika ili walioshikiliwa na nguvu za misingi hiyo wawe huru kwa uweza na nguvu za Roho wa Mungu katika jina la Yesu

Mfano; ukisoma kitabu cha matendo ya mitume (Mtdo 16: 19-26) utaona habari ya watumishi wa Mungu waliokuwa wakihubiri habari njema (Paulo ma Sila) wakikamatwa, wakapigwa bakora na kutupwa gerezani kwa kufungwa miguu.
Wakiwa ndani ya gereza walianza kumwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu  na kumwabudu licha ya wafungwa wenzao kuwashangaa. Mungu aliyehai alishuka katika Roho wake ili kuwasaidia, kuwakomboa na kuwatoa katika kifungo cha maisha yao ya utumishi yaani gerezani kwa kuachilia nguvu zake katika misingi ya gereza. Mstari wa 16:26, Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa, unasema Mungu aliachilia nguvu za kutetemesha misingi ambayo gereza limejengwa juu yake. Kwa jinsi ya kiroho lile halikuwa gereza la kawaida bali ni nguvu iliyowakamata watumishi iliyokuwa  katika misingi ya eneo au gereza walilokuwemo, kwahiyo Mungu aliyehai alipiga nguvu ya  adui iliyokuwa katika misingi na kuiyumbisha mpaka eneo zima na jengo likatetemeka na kuvunjika na watu wa Mungu kuwa huru katika jina la Yesu aliye hai. Haleluya! haleluya!

05. 02. Kutikisa misingi

2Samweli 22:8, Ndipo nchi ilipotikisika na kutetemeka, Misingi ya mbinguni ikasuka-suka Na kutikisika, kwa sababu alikuwa na ghadhabu. Isaya 6:4, Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Zabri 18:7, Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu.

Msingi wa nyumba au jengo ndio ambao umebeba au umeshikilia nyumba au jengo zima kwa maana hiyo, msingi ukitikisika lazima mipasuko ianzie chini katika misingi kupanda katika kuta za jengo zima, na mpasuko inayotoka katika misingi ni mibaya sana, inagharimu na ina madhara makubwa. Neon la Mungu aliyehai liko hai na lina nguvu ndani yake ambayo unapotamka Neno linaambatana na uhai ulio ndani yake, nguvu ya ajabu, utiisho na mamlaka kuelekea lilipoelekezwa ili kutikisa misingi.
Kwaiyo, kama kwa namna ya kiroho kila kitu au jambo lolote lina chanzo chake, chimbuko au kiini yaani msingi ambao ulisimikwa au ulijengwa ili uwe mwendelezo wa kumiliki na kutawala mfumo wa maisha na hali ya maisha ya watu walio ndani ya msingi huo. Msingi huo ukiguswa au ukitikiswa lazima na mifumo ya maisha ya watu au hali za maisha ziathiriwe kabisa, ziguswe au lazima kutokee vitu kadhaa.
Mungu aliye hai anapotaka kuwasaidia au kuwakomboa na kuwatoa watu wake waliofungwa katika msingi wa ufalme wa shetani kwa njia mbalimbali kama; sadaka, viapo, maagano na laana, anaachilia nguvu zake katika msingi wa mfumo unaowatesa au chanzo cha kifungo hicho ili kiachie na watu wawe huru katika kuishi kwao.
Mfano; kitabu cha Yoshua 6:20, Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji.
Kinatueleza juu ya mpango wa Mungu juu ya kuwakomboa watu wake waliokuwa ndani ya Yeriko akiwemo mtumishi mwanamke Rahabu aliyekuwa kahaba. Mungu alimpa mtumishi wake Joshua namna ya kufanya au maelekezo ya kuyafanyia kazi ili kumkaribisha Mungu katika Roho wake na nguvu zake ili kuwasaidia na kuwatoa ndani ya ufalme, kuta, vifungo na ngome ya Yeriko. Joshua na wana wa Israeli walifuata maelekezo waliyopewa ya kuzunguka Yeriko huku wakibeba sanduku la Bwana na tarumbeta  mara moja kwa siku sita na siku ya saba walizunguka ukuta wa Yeriko mara saba kwa kupiga tarumbeta na kelele au kupaza sauti kwa Mungu wa Israeli, na alishuka kwa nguvu katikati yao. Mungu aliposhuka katika Roho wake wa nguvu alielekeza nguvu zake katika misingi wa ukuta wa ngome au mji wa Yeriko, ili kupiga nguvu za miungu ya Yeriko iliyokuwa inamiliki na kutawala eneo hilo. Nguvu za Mungu ziliachiliwa katika eneo au juu ya msingi uliokuwa umekamata, umebana, umeshikilia, umefunga na kuwatumikisha watu wa Mungu wa israeli katika matendo ya uovu kama Rahabu-ukahaba kwa muda mrefu, Mungu alitikisa misingi katika ulimwengu wa roho na kuta, vifungo na minyororo zikatikisika hadi kuvunjika,  kubomoka na kuwaachilia watu wa Mungu wawe huru.
Maombi ya toba yanavyofanyika katika misingi, Mungu aliye hai katika Kristo Yesu anaachilia nguvu katika Roho ambazo zinalenga moja kwa moja kutikisa misingi au kiini cha mifumo fulani au hali fulani ya maisha ili kuwaokoa na kutawala watu wake ili wawe huru ndani ya Kristo Yesu.

05. 03. Kuwasha moto na kuchoma misingi

Mungu aliye hai katika Roho yake anaweza kujibu maombi ya waombaji au watumishi wake kwa kuwasha moto na kuichoma misingi ili iyeyuke, iteketee, ifutike na kuondolewa kabisa.
Moto katika Roho wa moto, unapoachiliwa katika eneo au ardhi ambayo imesimikwa na imejengwa misingi ya nguvu za giza, moto unalenga kuchoma, kutekeza na kulamba maneno ya viapo, laana na maagano ya dhambi, hatia na uovu ilivyopelekea giza kuwa na uhalali, pia moto unalamba, kuchoma na kuyeyusha vifungo mbalimbali, kamba na mitego ya giza ili msingi uondolewe uhalali wake na ufutike kabisa na kuyeyuka ili mfumo wa maisha na hali ya maisha ya watu wa Mungu wakombolewe na kuwa huru katika Kristo Yesu.
Moto anaouachilia Mungu katika Roho ya moto unakwenda kuchoma, kuteketeza na kuunguza mizizi ya misingi iliyo katika eneo fulani inayokamatilia, inayotawala na kutumikisha watu ili kuiondoa na kuondoa ufalme wa adui ili Mungu ajijulishe katika moto kuwa yeye ndiye Mungu peke yake.
Mfano; habari ya Mungu kujibu kwa moto na ishara kuu tunaipata vizuri katika kitabu cha 2Wafalme 18:30-39 Mungu alijibu kwa moto ili kuchoma, kuteketeza na kuunguza madhabahu na nguvu za bahari ili kujijulisha, kujidhirisha na kujifunua kuwa yeye ndiye Mungu peke yake katika Israeli. Haleluya!! Haleluya!! mtu wa Mungu aliye hai.

05. 04.  Kufunua na kufichua misingi

2Samweli 22:16, Ndipo ilipoonekana mikondo ya bahari, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Kwa kukemea kwake Bwana, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwake. Ayubu 4:19, Je! Si zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo, Ambazo misingi yao i katika mchanga, Hao waliosetwa mbele ya nondo! Ezekieli 13:14, Ndivyo nitakavyoubomoa ukuta mlioupaka chokaa isiyokorogwa vema, na kuuangusha chini, hata misingi yake itafunuliwa; nao utaanguka, nanyi mtaangamizwa katikati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. Mika 1:6, Kwa ajili ya hayo nitafanya Samaria kuwa kama chungu katika shamba, na kama miche ya shamba la mizabibu; nami nitayatupa mawe yake bondeni, nami nitaifunua misingi yake. Zabri 18:15, Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee Bwana, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.
Ufalme wa giza umefitinika na kusitirika kwa namna ambavyo unatenda kazi zake katika giza kwa kujificha au katika siri, hivyo hata sadaka, viapo, maagano na laana vinavyotoa uhali wa kuwepo kwa ufalme wa giza hufanyika kwa siri. Njia  mojawapo ya kumfukuza shetani mahali ni kumfunua na kumweka wazi na siri zake zilizofichika kujulikana kwa uwazi ili ahaibike, ahame au atoke katika eneo alilokuwa amejificha.
Ufalme wa Nuru katika Yesu aliye hai hutenda kazi yake katika Nuru, Kweli na waziwazi. Kristo ambaye ni Nuru alikuja ili kuangaza mambo yote hata yaliyo sirini na gizani ili kuyafichua. Mojawapo ya kazi ya Mungu aliye hai katika mwanae aliyejaa neema na Kweli katika Nuru ni kufunua na kufichua misingi ya ufalme wa giza iliyoko katika eneo fulani.
Misingi mingine inafichwa katika mchanga na udongo au ardhi. Mfano, kuchimba ardhi ndani ya shamba, nyumba au katika njia panda ili kuweka madawa au matambiko kwa hiyo kazi ya Mungu aliye hai ni kuifichua, kuchimbua ardhi ili vitu vilivyowekwa ndani ya ardhi viwe wazi na watu wawe huru katika Kristo Yesu

05. 05. Kubomoa misingi

Njia nyingine ambayo Mungu akiitwa na kukaribishwa na watu wake (waombaji) kwa njia ya maombi kwa kuachilia na kunyunyizia damu ya Yesu katika misingi ni kubomoa msingi wa nguvu ya ufalme wa shetani uliosimamishwa mahali fulani.
Mtu anaweza akaamua kubomoa msingi wa nyumba yake kwa sababu alizonazo yeye kama; kupanua msingi wa nyumba, kuuondoa  uliokuwepo ili kujenga kwa upya au kujenga msingi mpya au kuondoa kabisa ili eneo liwe wazi kwa taratibu za kawaida kwa kutumia nguvu kama mitambo n.k.
Mwombaji anapoingia katika limwengu wa roho ili kuathiri mambo yaliyo rohoni, mfano kunyunyizia damu ya Yesu katika misingi ya mfumo wa maisha, nguvu iliyo ndani ya damu ya Yesu inaachiliwa na inapata nafasi ya kujidhihirisha ili kupiga na kuvunja na kubomoa ngome za ufalme za giza sawasawa na Neno la Mungu aliye hai.
Mungu unapomwomba anatuma Neno la kukusaidia, kukutoa mahali ulipo, kukuvusha na kukupa maelekezo ya kufanya ili upige hatua ambalo ndani yake kunakuwemo na nguvu ya utendaji juu ys jambo ambalo ilo anaeno limetumwa kwalo. Mfano, Yeremia 1:9-10

05. 07. Kuifungua misingi ilipofungwa na iliposhikiliwa

Yeremia 1:9-10, Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda
Wakati wa ujenzi wa msingi wengine huwa wanaweka nondo nzito na wanazisuka vizuri, zege nzito ili kutengeneza msingi wa nyumba ulio imara, ambao ukitaka kuubadilisha au kuubomoa inakugharimu kutulia na kuufumua taratibu ili kuweza kuuondoa kikamilifu au kutumia mitambo ya kisasa ili kuvunja, kuharibu na kubomoa msingi huo.
Katika ulimwengu wa roho  kwa uteka wa nguvu za giza uliochukua muda au mrefu uliokomaa na wenye nguvu ambao umejengeka na kujiimarisha kwa uimara wa kutosha, unahitaji kutimuliwa taratibu kwa kunyunyiza damu ya Yesu ili ipenyeze mpaka ndani ili kufunga kamba zote, nyaya, mitego, tanzi, vyuma na vifungo vyote ili kilichokamatiliwa ndani yake kiwe huru kwa damu yaYesu Kristo ili kuwafaidia watu wa Mungu.
Misingi inaposimikwa, au inapojengwa inaweza ikakazwa mahali fulani ambapo wakati wa kuifungua inahitaji utulivu na nguvu ya ziada ili kuifungua .
Luka 19:29-36, ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi, akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa. Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji. Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda? Wakasema, Bwana ana haja naye.
Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani.

Tunaona Yesu akiwaagiza wanafunzi kwenda kumfungua mwanapunda aliyekuwa amefungwa mahali fulani, huenda alifungwa na kamba ngumu ambazo hazikatiki kiurahisi na haziwezi kutoka kirahisi katika eneo alipokuwa amefungwa, huenda alikuwa anataka na analazimisha kutoka lakini kamba hazimwachii, hata hapati msaada wowote wa kumsaidia kumfungua ili awe huru, amekaa hapo kwa mda mrefu mpaka amechoka, pengine hata majani yaani chakula kimeisha ilo eneo, kila msimu unamkuta hapo na kumwacha hapohapo, pengine amekonda mpaka amekata tama, anajiuliza maswali mengi juu kesho itakuwaje, hajui hata nani aliyefunga na sababu za kumfunga nazo hajui, nap engine haoni hata kosa.  Ooooh lakini ujio wa Bwana Yesu katika maisha yake !!!!! (sema ujio wa Yesu)
Yesu aliwapa maelekezo ya namna ya kumfungua, namna ya kujibu ikiwa wataulizwa kwanini wanamfungua; aliwaelekeza na mahali alipokuwa kule ndani ya kijiji maana yake alipokuwa amefichwa, namna ya kumleta kwa Yesu, na sababu ya kumfungua na kumleta kwa Yesu ni kwa sababu anataka kumtumia yaani Bwana ana haja naye.
Wapo watu wengi waliofungwa na kamba na vifungo mbalimbali katika mti au kisiki/shina walipofungiwa yaani katika misingi kwa njia ya laana, viapo, maagano na sadaka hivyo, Yesu anataka kuwafungua, kuwaokoa na kuwatoa ili wawe huru na watumike katika yeye.
Kwa hiyo Mungu ukimkaribisha katika misingi yako binafsi, familia, ukoo, taasisi na eneo iliyokamata na kufunga hali ya maisha yako, jambo mojawapo analoweza kufanya ni kukufungua na kukutoa katika misingi ya uteka uliyomo hata kama unamwombea ndugu au rafiki yako  ili uwe huru katika yeye Kristo Yesu, uwe huru ndani ya Yesu katika yote.

1 comment:

  1. vizuri sana mtumishi, hii ni kazi njema ya kuwafundisha watu. kama isemavyo zaburi(82:4- 5)4 Mwokoeni maskini na mhitaji; Mwopoeni mikononi mwa wadhalimu.5
    Hawajui wala hawafahamu, hutembea gizani; Misingi yote ya nchi imetikisika.

    ReplyDelete